MKUU
wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe ameagiza kukamatwa kwa watu
watatu wakiwamo raia wawili wa China kwa kuendesha mgodi wa mawe ya
kutengenezea marumaru kinyume na sheria.
Aidha, wamebainika kukwepa kodi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 92.Dk.
Kebwe pia amewasimamisha kazi maofisa wawili wa halmashauri hiyo kwa
kushindwa kufuatilia mapato kwa kipindi cha miaka sita mfululizo.
Alitoa
maagizo hayo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya,
baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mgodi wa mawe ya
kutengenezea marumaru, unaoendeshwa na kampuni ya Zhan Fa Construction
Material Group, Kijiji cha Maseyu, Tarafa ya Mikese, wilayani Morogoro.
Alisema
amelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kubaini kampuni hiyo
ikiendesha mgodi huo kinyume na sheria baada ya kufungiwa na serikali
tangu mwaka 2010, lakini bado waliendelea na uzalishaji, na kuagiza
kukamatwa kwa wafanyakazi watatu wa mgodi huo.
Aliagiza
kukamatwa kwa Shiqing Liang ,Wang Jun na Hilary Paul, na kuwasimamisha
kazi maofisa wawili wa halmashauri hiyo akiwamo Ofisa Mipango, Joel
Mkesela na Ofisa Biashara, Denis Lyepa, kwa kushindwa kufuatilia mapato
ya halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka sita mfululizo.
Wakati
akitembelea maeneo mbalimbali ya mgodi huo, alibaini kuendelea kwa
shughuli nyingine za usafishaji wa madini ya dhahabu kinyume na sheria,
na kukuta mifuko ya sandarusi maarufu kama viroba ikiwa na mchanga
unaodhaniwa kuwa na madini ya dhahabu, tayari kusafirishwa.
Viongozi
mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro akiwamo Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, Kibena Kingo na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini
Mashariki, Omary Mgumba, walisema mgodi huo ulikuwa ukikwepa kodi na
kuwaathiri katika mapato ya halmashauri.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment