Viongozi
serikalini wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu, wameombwa na Rais John
Magufuli, kuvumilia machungu wakati wa uongozi wake, kama ambavyo
wananchi walivyovumilia tangu Uhuru.
Amesema
hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza
ya juu (flyover) nchini Tanzania, inayojengwa katika makutano ya
Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere, eneo la Tazara, kwa ufadhili
wa Serikali ya Japan.
Machungu
hayo kwa mujibu wa Rais Magufuli, yataanza kuonekana wakati wa
utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya kwanza kwa Awamu ya Tano, ambayo
fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka asilimia 27 za bajeti iliyopita,
hadi kufikia asilimia 40.
Machungu yenyewe
Ili
kufanikisha dhamira hiyo ya Serikali, Rais Magufuli alisema katika
bajeti hiyo inayotarajiwa kupelekwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, litakaloanza vikao vyake Dodoma wiki ijayo, machungu hayo
yataanza kuonekana kwani fedha za chai, semina na safari, zimekatwa na
kujaziwa katika fedha za maendeleo.
Kutokana
na makato hayo, Dk Magufuli amesema kutakuwa na machungu hasa kwa
watendaji wa Serikali na kuwaomba mawaziri na makatibu wakuu ambao
alisema walikuwa wakifaidi matunda ya Uhuru, wavumilie machungu hayo
kwani wananchi wa maisha ya chini wamevumilia machungu kwa muda mrefu.
“Wananchi
wamechoka kutuona sisi viongozi tunafaidi matunda ya Uhuru wa nchi
tangu Uhuru na wao wakiwa wasindikizaji halafu wao tunawaomba kura na
wakishatupigia tunawasahau,” alisema na kuongeza kuwa anataka wananchi watoke kwenye machungu na sasa wawe ‘watamu’ kwa maendeleo.
Magufuli
alisema lazima viongozi wabadilike na kurudi kwa wananchi wa maisha ya
chini na hiyo itakuwa sadaka kwa kuwapa madaraka kwani wananchi wanyonge
wameteseka siku nyingi.
Wasiovumilia
Alisema
waliokuwa wamezoea chai, safari na posho za ovyo kama wanaona au
wanafikiri hawawezi kufanya kazi bila hizo chai, waache kazi mara moja
kwani sasa fedha zinazokusanywa za walipa kodi wanyonge, zitaenda
kutatua matatizo yao ya hospitali, barabara na kununua ndege za
Serikali.
Pia
alionya kuwa katika uongozi wake hakuna mtu atakayekwenda kinyume na
utaratibu na kisha ‘akachomoka salama’ na kama kuna anayeona hawezi
ajiondoe mwenyewe kwani Watanzania wanaendelea kumuombea.
Dk
Magufuli alisema wananchi wote bila kujali vyama vya siasa, wanalilia
maendeleo na maendeleo hayana chama, kwani wananchi wamechoka ‘machama
chama’, wanataka kwenda mbele, hivyo hakuna sababu ya kubaki nyuma na
kubishana kwa mambo ya chama chama, wakati uchaguzi umepita na
aliyeshinda ni yeye ambaye ni CCM.
Machungu ya zamani
Ingawa
Rais Magufuli alisema machungu hayo yataanza kuonekana katika Bajeti
inayotarajiwa kuanza kujadiliwa na Bunge litakaloanza vikao wiki ijayo,
lakini watendaji wa Serikali walianza kuona machungu ya msimamo wake
tangu alipoingia madarakani Novemba mwaka jana.
Itakumbukwa
kuwa Novemba 7, mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, katika mkutano
wake wa kwanza na watumishi wa ngazi za juu wa Serikali, hasa makatibu
wakuu, naibu makatibu wakuu na watendaji wengine wakuu wa Serikali, Rais
Magufuli alitangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo
atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine.
Mpaka
sasa Rais Magufuli amehakikisha shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje
ya nchi zinafanywa na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha
nchi, ambapo watumishi watasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura
na pamoja na udharura wake, lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu
Kiongozi au Makamu wa Rais.
Katika
kile kinachoonekana kuwa hatanii, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa
kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambao walikaidi agizo lake la kuwataka
watumishi wa umma kutosafiri nje ya nchi.
Watumishi
hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas
ambao walisafiri kwenda nje ya nchi, licha ya kutokuwa na kibali cha
safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Aidha
ndani ya siku zake 100 za kwanza tangu alipoingia madarakani, tayari
Serikali yake ilikuwa imeshawafukuza kazi vigogo zaidi ya 70 kwa tuhuma
mbalimbali ikiwamo za ufisadi.
Novemba
9, mwaka jana, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza
kuwa Rais Magufuli aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru
ambapo fedha zilizookolewa aliagiza zipelekwe katika mradi wa kupanua
kipande cha barabara kutoka Morocco mpaka Mwenge katika wilaya ya
Kinondoni.
Hatua
hiyo ilitanguliwa na kupunguza fedha za sherehe ya kupongezana ya
wabunge, ambazo alizielekeza kwenda kununua vitanda, magodoro na mashuka
kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hivi
karibuni alipokuwa akiapisha wakuu wa mikoa, aliwataka kwenda kuwasaka
watumishi hewa na kutangaza idadi yao, ambapo aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, aliposema hajakuta watumishi
hewa wakati wapo, Dk Magufuli hakusita kumuondoa mwanzoni mwa wiki hii,
ingawa hakuwa amemaliza hata mwezi tangu aripoti kazini.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment