Samia, ambaye pia aliweka bayana kuwa
chama hicho tawala kilikumbana na upinzani mkali kwenye Uchaguzi Mkuu
uliopita, alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua semina ya wabunge,
madiwani na viongozi wa CCM wa Mkoa wa Dodoma na baadaye kwenye kikao
cha UWT.
Akiwa katika mkutano wa Baraza la UWT, Samia aliwataka
viongozi wa jumuiya hiyo kutoa mafunzo maalumu kwa wabunge wapya ili
waweze kupambana na wapinzani.
Alihoji ni mambo gani wanayofundishwa wabunge hao wanawake katika kutimiza wajibu wao ndani ya Bunge.
“Tunawafundisha nini ama (tunawafundisha) wakajibu vijembe tu, au wakaseme nini kama wabunge waliotoka UWT?” alihoji.
Samia
amesema hayo wakati maneno ya kashfa na vijembe yakizidi kutamalaki
ndani ya Bunge na kusababisha kelele, majibizano na wakati mwingine,
wabunge wa upinzani kutolewa nje au kususa.
Juzi, wabunge
wanawake wa vyama vinavyounda Ukawa walisimama na kupaza sauti kupinga
kitendo cha Mbunge wa CCM, Goodluck Mlinga kudai kuwa wanawake wa
upinzani hawawezi kupata nafasi za kisiasa bila ya kuitwa “baby”, neno
la Kiingereza linalotumika kumaanisha mpenzi.
Naibu Spika Dk
Tulia Ackson aliyekuwa anaongoza kikao hicho, alilazimika kuwaamuru
wabunge hao waende nje ya ukumbi baada ya kukaidi amri yake ya kuwataka
wakae vitini.
Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya mbunge
mwingine wa CCM, Augustine Holle kudai kuwa wabunge wawili wa Chadema,
Tundu Lissu na John Mnyika wana mafaili kwenye Hospitali ya Mirembe ya
mjini Dodoma ambayo inahudumia wagonjwa wa akili na Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili (MNH).
Kauli yake ilisababisha Mbunge wa Ukonga
(Chadema), Mwita Waitara kunyanyuka kwenye kiti chake na kuanza kumfuata
mbunge huyo wa CCM kwa kile kilichoonekana kwenda kupambana naye,
lakini hakufanikiwa na kuamriwa aende nje.
Mara kadhaa mbunge
mmoja anapokuwa anachangia hoja inayogusa upande mwingine, wabunge
huwasha vinasa sauti vyao na kutoa maneno ya kejeli, kashfa na dhihaka
yanayosababisha Bunge kujaa kelele za mara kwa mara.
Samia na
upinzani
Akizungumza kwenye kikao na viongozi wa CCM wa mkoa, Samia
alisema katika kipindi cha miaka 20 tangu siasa za vyama vingi
ziliporejeshwa, vyama vya upinzani vimejijenga na sasa vinaweza
kukabiliana na Serikali.
“Bila kusahau kwenye Bunge tuna wenzetu
kutoka vyama vya upinzani ambao wamekua vya kutosha, wamepevuka vya
kutosha,” alisema Makamu wa Rais.
“Katika miaka 20 ya vyama
vingi, upinzani umezalisha watu makini ambao wako tayari kupambana na
Serikali. Je, wa kwetu tumewaandaaje katika kupambana nao?”
Kuhusu
Uchaguzi Mkuu uliopita, Samia alisema CCM ilipata upinzani mkali
kutokana na vyama vya upinzani kuimarika na pia chama hicho tawala
kukumbwa na mgawanyiko.
“Kukosa umoja ndani ya chama chetu
kulifanya adui akaingia akiwa amejiimarisha na kweli alisumbua sana
kwenye uchaguzi na ndiyo maana tunasema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa
2020 yaanzie sasa,” alisema Samia.
Alisema kuna baadhi ya viongozi ndani ya chama ambao hawakuwa waaminifu akieleza kuwa ndiyo waliofanya uchaguzi huo uwe mgumu.
CCM
ilipoteza makada wawili waliowahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu, Edward
Lowassa na Frederick Sumaye waliohamia upinzani na kuwa tegemeo kubwa
kwenye kampeni, Lowassa akiwa amepewa nafasi ya kugombea urais na Sumaye
akitegemewa kwa hoja zake kwenye mikutano mingi.
Pia, mawaziri,
wabunge na madiwani wa CCM walikihama chama hicho na kuimarisha
upinzani uliofanya mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kushinda kwa
asilimia 58.2, ambao ni mdogo kwa chama hicho kulinganisha na chaguzi
zilizopita.
Aliwataka viongozi wa chama kuondoa woga na badala
yake waisimamie Serikali kwa kuwa ilani inayotekelezwa ni ya CCM na
akawataka wafanye kazi hiyo kwa kushirikiana na watu wa chini yao.
Akiwa
kwenye mkutano wa jana, Samia alisema UWT haina budi kukaa na wabunge
hao na kufanya nao mafunzo maalumu kwa sababu kazi kubwa ya makundi ya
wanawake ndani ya mabaraza ya kutunga sheria ni kutetea masilahi yao.
Sophia
Simba ataka wakuu wa Wilaya
Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba alimuomba Makamu wa
Rais kuwaombea kwa Rais Magufuli kuwapa kipaumbele wanawake wengi katika
nafasi za ukuu wa wilaya wakati atakapofanya uteuzi akisema wana uwezo
mkubwa wa kutumikia nafasi hiyo.
Alisema UWT itakuwa na shughuli
mbalimbali ambazo itafanya kwa muda wa siku tatu mkoani Dodoma, ikiwa ni
pamoja na kumpongeza Samia ambaye pia ni mmoja wa wadhamini wa umoja
huo, kwa kuchaguliwa kwake kushika nafasi hiyo.
Majipu
yatatumbuliwa
Akizungumzia suala la kutumbua majibu, Makamu wa Rais
alisema kazi hiyo itaendelea hadi wahakikishe Taifa linarudi kwenye
mstari na akaomba viongozi wote kuwa makini katika sehemu zao za kazi.
“Hapa napo niseme ukweli kuwa majipu siyo tu yapo huko juu, hata katika
ngazi za chini yapo tena kuanzia kwenye chama na Serikali. Anzeni
kuyatumbua kwa kuwa mkichelewa mtatumbuliwa ninyi,” alisema.
Aliwataka kujiandaa kwa kuwa “mzee wa kutumbua majipu” yupo karibu kukabidhiwa chama ambacho alisema kina majipu.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment