Serikali imetangaza kuokoa kiasi cha Sh15.4 bilioni katika kipindi cha kuanzia Machi hadi Aprili 24 ambacho kingelipwa kwa watumishi hewa 8,236 ambao wamebainika hadi sasa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Utawala Bora, Angela Kairuki aliliambia Bunge jana kuwa kazi ya kuwasaka
watumishi hewa bado inaendelea nchini kote.
Alisema watumishi hao wamebainika katika maeneo mbalimbali na kati yao 1,614 ni wa Serikali Kuu na 6,624 wa Serikali za Mitaa.
Waziri
alisema kuwapo kwa watumishi hewa kumewafukuzisha kazi maofisa 56 na
taratibu za kuwafungulia kesi mahakamani zinaendelea ikiwamo kutakiwa
kulipa hasara yote ambayo waliisababisha.
Alisema mapambano dhidi ya watumishi hewa ni endelevu ili kukomesha tabia hiyo inayolitia hasara taifa.
“Mheshimiwa
Rais alitangaza siku za hivi karibu na mtaona nami natangaza leo idadi
ikiwa juu kuliko aliyotangaza Rais na vyombo vingine vitaendelea
kutangaza maana tuko kwenye kazi kila siku,” alisema Kairuki.
Alitaja
changamoto kubwa katika wizara yake ni kuwa ni tofauti ya mishahara kwa
wafanyakazi ambayo inaonekana ni kubwa kati ya mtu wa chini na wa juu
yake, jambo alilosema Rais ameamua kulisimamia ili kulipunguza.
“Tofauti
ya mishahara ni kubwa, kuna baadhi ya maeneo mtu anatakiwa kupokea
mshahara wa miezi 50 au 30 ili aweze kumfikia mwenzake mwenye mshahara
mmoja tu,” alisema Kairuki.
Kuhusu suala la ajira, alisema
katika mwaka wa fedha wa 2016/17, Serikali imepanga kuajiri watumishi
71,496 kuanzia mwezi huu na akawataka waajiri kuacha kuwahamisha
watumishi endapo hakuna fedha za kuwalipa.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment