June 18, 2016

                             
 
Na.luqman maloto

INAUMA sana na inahuzunisha kupita kiasi. Mitandaoni kote jana habari ilikuwa Rehema Yusuf Chalamila ‘Ray C’ kuokolewa na polisi Kinondoni, Manyanya. Kwamba Ray C alikuwa katika hali mbaya baada ya kubwia unga kama kawaida yake. Ndiyo, Ray C amerejea tena kwenye michezo yake, tena kwa kasi kubwa.

Kwa hakika Ray C hakustahili kufika huku. Kiuno Bila Mfupa, mkali aliyetingisha kisawasawa kwenye Bongo Fleva. Mrembo mwenye macho yake ya kusinzia, sauti yake ya kubembeleza, DJ wa kwanza mwanamke Bongo. Mkali wa Bongo Fleva mwenye kiuno kama dondora, mwenyewe akasema ni Kiuno Bila Mfupa. Amekuwa wa kuokotwa na polisi baada ya kuzidiwa na uteja! Nimeweka alama ya mshangao si kwa kushangaa bali kwa tahayari. Ninayo maumivu yangu.

Niliushuhudia ubora wa Ray C, akiwa mwanamke ghali mno Bongo, mapedeshee na vigogo mbalimbali wakiumiza kichwa na wengine wakitapeliwa mamilioni ili kulipata penzi lake, lakini siku hizi anaokotwa kama kibinti ambacho hakijawahi kuwa na mbele wala nyuma hapa mjini.

Ray C mwenye nyumba zake, maduka ya nguo na vipozi, siku zote ungemuona kwenye gari lake akiendesha hata vioo hashushi, kipupwe kilifanya kazi yake vizuri. Ray C mwenye kupanda ndege kwenda kufanya ziara za nje na kurejea bila wasiwasi, leo anahitaji huruma, tena huruma kubwa.

Alikuwa anasafiri kwenda Uingereza, Marekani na nchi yoyote aliyopenda. Shopping zake Dubai na China, starehe zake Lagos, Nigeria na aliyekuwa boyfriend wake, Mwisho Mwampamba. Hivi sasa hata nauli ya kupanda basi la mwendokasi anaipata kwa kuungaunga. Usiwazie nauli ya kwenda Arusha au Mwanza.

Labda wengine, ila mimi sikuwa tayari kuushuhudia mwisho huu wa Ray C. Nilimuona akiwa na thamani yake. Aliogopwa na kunyenyekewa hasa. Inaumiza mno kuona kuwa mrembo yule gumzo la nchi na homa ya Jiji la Dar es Salaam, amekuwa wa kuokotwa tu. Hana thamani tena. Ndiyo ni teja wa kutupwa!

Ray C wa sasa si yule ambaye Mwisho alijidai kumpata baada ya kutoka Big Brother Africa ya kwanza mwaka 2003. Wakati huo wote wakiwika kwa usupastaa wao. Taifa likawainamia na kuwapa shangilio kuwa wao ni wapenzi (couple) bora mno kwa mastaa. Wakafuatiliwa na kumulikwa na vyombo vya habari kuliko hata couple ya Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ na Garder Gabriel Habash.

Huyu Ray C wa sasa, hafanani na yule ambaye alimtoa udenda prodyuza legend wa muziki na Mkurugenzi wa Studio za Bongo Records, Paul Matthysse ‘P-Funk’ ambaye alikuwa kwenye chati sana wakati huo. Mdachi wa Kibongo mwenye swaga zake, vile alivyo chotara na umaarufu wake, warembo akina Amber Rose wa Bongo wakashobokea penzi lake.

Kwa Ray C, P-Funk alizima zake. Akachachawa, Kajala Masanja akiwa kama mke wa Mdachi ‘Kinywele Kimoja’ akawakuta P na Ray C studio wakifanya yao. Ngumi zikapigwa pembeni ya vitendea kazi vya Bongo Records. Sijui kama Ray C wa sasa angewagombanisha P-Funk na Kajala. Maisha ya Rehema yamebadilika katika sura ambayo haivutii na zaidi inatesa mashabiki na familia.

Kilichomfika Ray C ni sawa ni ile hadithi ya tumbo niachie nimwachie Mandawa! Manenge alisema hivyo alipozidiwa na utamu wa chakula. Aliomba ikashindikana, mwisho chakula kikaisha.

Ray C naye anakemea, unga koma, nao haukomi, umemganda. Labda mimi niseme, wewe unga, hebu koma basi! Acha mazoea umwachie Ray C wetu awe huru na maisha yake.

Inauma sana. Mwishoni mwa Februari, mwaka huu, nilidamkia alfajiri kwenye mtaa mmoja nyuma ya Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.

Nilishikwa na ganzi kutokana na sikitiko la ajabu ambalo lilinipata. Ray C aliniumiza kumshuhudia! Hakika alitia huruma kumuona.

Ray C aliumiza wengi kabla lakini alileta matumaini makubwa pale alipopata uokovu kisha kutoa ushuhuda wa kuachana na madawa ya kulevya. Dah! Ray C karejea tena kuzimu.

Ndiyo kusema Ray C amejihukumu kifo, maana anatambua wapi alikuwa. Rais wa Nne, Dk. Jakaya Kikwete alimwokoa Ray C, akamrudisha tena kwenye maisha.

Siyo uongo kuwa Dk. Kikwete alimrudisha Ray C kwenye maisha kwa sababu alikuwa tayari kwenye mkondo wa kifo (death row) kutokana na kutopea kwenye madawa ya kulevya.

Nikiwa pale mtaani, nyuma ya Hospitali ya Mwananyamala, nilimshuhudia Ray C, akikimbia hovyo, nikauliza wenyeji pale wakaniambia: “Ndiyo zake kila siku, anaamka alfajiri anasema anafanya mazoezi. Ila siyo mazoezi, ni mambo yake hayo.”

Kabla ya hapo, nilipewa taarifa kuwa nikitaka kushuhudia vituko vya Ray C basi niamke muda huo, niende Mwananyamala.

Naomba uvute picha kama mimi. Tumvute yule Ray C (Rehema Chalamila) mwenye viwango vyake. Kumbuka wimbo Mapenzi Matamu, kisha ikumbuke video yake. Haya sasa, tumwangalie mtoto mzuri Ray C akiimba kwa sauti tamu ya kimahaba.

Sauti fulani hivi ya kutokea puani! Mtoto akawa analeta ladha nzuri ya Kipwani na vile mwenyewe alikuwa anainakshi sauti yake nzuri yenye mchujo wa koo na pua! Sasa tuseme mashallah!

Unakumbuka alivyokuwa anacheza? Jinsi nyonga yake alivyokuwa anaichezesha, na vile aliwezeshwa na Maulana ‘ka-kiuno’ kembamba! Basi jina lake maarufu likawa Kiuno Bila Mfupa!

Nyakati ambazo Lady Jaydee alikuwa malkia wa muziki wa kizazi kipya Bongo. Ray C alipotoa albamu yake ya pili mbona Jide na Ukomando wake wote alifichwa? Kumbuka ‘misongi’ Niwe na Wewe Milele na Si Ulinikataa, Ray C ni fundi jamani. Sijui kafikaje huku?

Mitaani, klabu, redioni, runingani, katika vyombo vya usafiri binafsi na umma pamoja na kwingineko, sauti ya Ray C ilitawala!

“Nataka niwe na wewe milele, nataka tuwe na watoto baby, nataka tuishi wote pamoja…” Ray C aliimba na kukonga nyoyo inavyotakiwa.

“Si ulinikataa bila sababu, ukaninyanyasa bila aibu, nimepata mwingine tabibu, sasa wanifuata nini…” Ray C alibamba inavyotakiwa!

Ray C alipotea lakini siku Jay wa Rhymes na AT walipomshirikisha kwenye wimbo Mama Ntiliye, aliwafundisha watu adabu. Ray C ni kichwa, fundi, mrembo na hatuwezi kupingana kuwa anavyo vionjo kamili vya kike!

Sifa zote hizo, sasa haya ya unga yanakuja vipi Ray C? Aliacha unga na akatangaza kupona, akawapa wengi matumaini. Rehema amerejea tena kwenye unga. Inauma sana ujue!

Tafadhali Rehema, wewe ni kioo kwa jamii yako, ukipata matatizo unaumiza wengi. Ujue kuna watu wanajifungia ndani wanalia kwa sababu yako. Kwa nini Rehema?

Labda ndiyo kama inavyonenwa kuwa mzoea kunyonga vya kuchinja haviwezi. Hii ni methali yenye tafsiri kwamba anayeishi bila utaratibu hata siku moja hawezi maisha yenye ustaarabu.

Kizungu kinazungumza: “He who likes to eat cows hump will not fail to grow fat.” Kiswahili kinajibu: “Mtegemea nundu haachi kunona.” Ray C, nini kilikupata mpaka ukarejea kwenye unga?

Kwa marejeo hayo ya matumizi ya unga, ndiyo kusema ile kazi kubwa aliyoifanya Dk. Kikwete ya kumuokoa kwenye uteja imekuwa kazi bure, maana sasa Ray C ni teja la kutupwa.

Kama Waswahili wanavyosema “mazoea ni papai kwa kijiko” ndivyo Ray C sasa alivyorejea maisha yake ya uteja kikamilifu, haoneshwi njia, kwani kona zake zote anazijua na anazipita kitaalamu kabisa.

Hivi sasa staa huyo wa Bongo Fleva, mwenye sifa ya kuwa DJ wa redio wa kwanza mwanamke nchini, anahitaji msaada wa huduma muhimu ili kumuokoa.

TATIZO NI METHADONE

Methadone ni dawa inayompa mtumiaji wa madawa ya kulevya hisia zilezile ambazo huzipata baada ya kutumia mihadarati lakini wakati huohuo hupata nafuu ya kimwili.

Kwa kawaida methadone huujenga mwili na kumsaidia mtumia madawa ya kulevya kisaikolojia, hivyo hata kama alikuwa amekonda hunenepa hata kupita kiasi, na ndiyo maana Ray C aligeuka bonge.

Wataalamu walifanya uchunguzi na kubaini kuwa ni vigumu mno kwa mtumia madawa ya kulevya kuacha haraka, hivyo kuona methadone inaweza kusaidia kwa sababu teja anapoitumia hupata ‘stimu’ zilezile za kubwia mihadarati.

Kutokana na sababu hiyo, zipo taarifa kuwa Ray C alipokuwa anakwenda kwenye kliniki yake ya mihadarati (rehab) katika Hospitali ya Mwananyamala, Kinondoni, Dar es Salaam, alikuwa siyo mvumilivu wa foleni.

Imebainishwa kuwa kutokana na kutokuwa mvumilivu wa foleni, Ray C alikuwa anasusa na kuondoka bila kupata dozi yake ya methadone.

Kwa vile Ray C ameshaathirika mno kwa mihadarati, ni vigumu kwake kuishi bila stimu, hivyo alipokuwa anapokosa kabisa madawa hupata ile hali ya uzoba ambayo inafahamika kama alosto.

Kutokana na alosto hiyo, Ray C alikuwa anakwenda mitaa ya Kinondoni, ambako alikutana na wauza unga ambao walimuuzia na kubwia.

Kwa utaratibu huohuo wa kwenda Kinondoni kununua unga na kubwia kila alipoona Hospitali ya Mwananyamala kuna foleni, taratibu lakini kwa uhakika zaidi (slow but sure), Ray C alijikuta anarejea zama zake za uteja.

Kutokana na kile ambacho kipo, ni kwamba awali haikuwa rahisi kumtambua Ray C kuwa amerejea uteja wake, lakini kuna mabadiliko ya hapa na pale aliyaonesha.

SIKITIKO KWA RAIS KIKWETE

Dk. Kikwete alijitolea hasa kumsaidia Ray C katika kipindi ambacho alipoteza kabisa uelekeo wa maisha kutokana na kutopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

Akiwa madarakani, Dk. Kikwete aliona mateso ya Ray C mitandaoni, hivyo kuagiza wasaidizi wake wamtafute kisha kumfanyia utaratibu wa tiba na uangalizi mpaka alipopona na kunenepa.

Rais Kikwete ana miezi saba tu tangu alipoondoka Ikulu na kumwachia Rais wa sasa, Dk. John Pombe Magufuli, hivyo anapopata taarifa za mabadiliko ya afya ya Ray C, bila shaka atakuwa anapata masikitiko makubwa.

TUMUOMBEE

Hakuna zaidi ya kumuombea Ray C, lakini kwa uamuzi wake wa kurejea matumizi ya unga, hakika ni sawa na kujihukumu kifo, maana mwenyewe kipindi kile alipotangaza kupona uteja alisema alinusurika kwenye mdomo wa kifo.

Kwa kasi ya matumizi ya unga ambayo Ray C anakwenda nayo, ni wazi kuwa anajitanguliza kaburini. Na bila kumung’unya maneno, ameshapoteza kila kilichokuwa kinampa thamani. Mungu akimnusuru, atakuwa na kazi kubwa mno kurejesha heshima na thamani yake. Haya yote kuhusu Ray C, binafsi sikuwa tayari kuyashuhudia.

Ndimi Luqman Maloto

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE