Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Jimbo la Bunda, Mkoani Mara Bi. Janeti Mayanja
amepokea madawati 90 yalitolewa na Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bi. Ester Bulaya, ambapo hapo
awali madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo hilo walikataa
kupokea madawati hayo baadaya ya kuwa yameandikwa jina la mbunge huyo
pamoja na kuwa yamenunuliwa na fedha za Mfuko wa Jimbo.
Akizungumza
leo kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mayanja alisema kuwa amepokea
madawati hayo jana Agosti 12 kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Ester
Bulaya baada ya kufutwa jina lake, ambapo madawati hayo tayari
yamewasilishwa katika shule tatu zilikuwa na uhaba.
“Tulifanya
kikao na Mbunge Bulaya na tukakubaliana kuwa ni vyema majina yake
yakafutwa katika madawati hayo kwa vile yalinunuliwa kwa fedha za Mfuko
wa Jimbo, lakini endapo mbunge atapenda kutupa madawati atakayonunua
kwa fedha zake binafsi na kuandika majina yake hapo tutapokea kwa vile
bado kuna tunauhitaji katika jimbo letu” alisema Mkurugenzi Mayanja
Alifafanua
kuwa fedha zilizotumika kununua madawati hayo zilikuwa ni fedha za
Mfuko wa Jimbo zinazotokana na ruzuku ya Serikali ambazo matumizi yake
hupangwa na Ofisi ya Mbunge.
Madawati hayo 90 yalisambazwa katika
shule tatu za Msingi zilizopo katika Jimbo la Bunda zilizokuwa na uhaba
wa madawati ambazo ni Nyatwali, Nyerere na Ligamba, zilizopewa
madawati 30 kwa kila moja.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment