Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) inatarajia kufanya mkutano wake wa 32 Septemba 22 hadi 24 mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa ALAT Stephen Mhapa amesema mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na changamoto na mafanikio ya jumuiya hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 hadi 2015.
“Mkutano huo utalenga kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za jumuiya kwa kipindi cha Julai 2015 hadi Juni 2016, pia tutajadili taarifa ya fedha, ukaguzi wa hesabu za jumuiya na makadirio ya mapato na matumizi yake kwa mwaka 2016/17,” amesema.
Amesema kauli mbiu ya mkutano huo imejikita katika kutimiza malengo endelevu ya ulimwengu pamoja na ukuaji wa miji iliyosalama.
“Kauli mbiu yetu ni Halmashauri zisipowezeshwa kwa rasilimali utekelezaji wa malengo endelevu ya dunia na agenda ya miji hautawezekana, ” amesema.
Amesema ili halmashauri ziwe na mafanikio, inahitajika juhudi za makusudi katika upelekaji wa rasilimali za kutosha katika serikali za mitaa.
Domina Feruzi, Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Serikali kutoka benki ya NMB ambayo ndiyo mdhamini mkuu wa mkutano huo, amesema NMB imeudhamini mkutano huo kwa kiasi cha Sh milioni 206.
“NMB imeudhamini mkutano huo kwa kuchangia sh milioni 150 kwa ajili ya gharama za maandalizi ya mkutano huo, na milioni 56 kwa ajili ya kununua zawadi ya trekta kwa viongozi wa halmashauri zilizofanya vizuri, ” amesema.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Musoma mkoani Mara.