September 12, 2016

Kitovu cha kijeshi na uchumi cha taifa hilo vililengwa na hujuma za kundi la kigaidi la al-Qaaidah. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa ardhi ya nchi hiyo kushuhudia hujuma za adui wa nje baada ya kupita miaka 189. Aina ya shambulio hilo, nyenzo zilizotumika kufanyia shambulio lenyewe, maeneo yaliyolengwa na ukubwa wa maafa ya roho za watu na hasara ya mali iliyosababishwa na hujuma za Septemba 11 zilibadilisha siasa, uchumi na utamaduni wa Marekani; kiasi kwamba, tunaweza kuyagawa matukio na hali ya Marekani katika vipindi viwili, cha kabla na baada ya Septemba 11.
Ndege za kijeshi za Marekani zikidondosha mabomu nchini Afghanistan mwaka 2001
Hata hivyo isisahaulike kwamba hadi sasa kuna dhana nyingi kuhusiana na tukio hilo huku baadhi ya maswali yakiwa bado hayajapatiwa majibu. Pamoja na kutafakari kuhusu nini kilijiri asubuhi ya tarehe 11 Septemba na watu gani waliohusika katika operesheni hizo, athari za tukio hilo ndizo ambazo zimekuwa na umuhimu zaidi kwa jamii ya walimwengu. Baada ya tukio la Septemba 11, 2001 ulimwengu uliingia kwenye kipindi kisichokuwa na mlingano katika vita, mauaji na machafuko. Katika radiamali yake serikali ya wakati huo ya Marekani iliingia katika vita vya kile ilichodai kuwa ni kupambana na 'ugaidi' na moja kwa moja ikazishambulia nchi mbili za Afghanistan na Iraq. Sambamba na uingiliaji huo kulianza pia operesheni za kijeshi kwa lengo la kukabiliana na mtandao wa ugaidi duniani. Wakati huo, madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yakakanyaga wazi wazi mipaka iliyoainishwa katika kuchunga faragha ya mtu binafsi na kadhalika sheria za haki za binaadamu na sheria za kivita katika vita vyao hivyo dhidi ya ugaidi. 
Askari wa Marekani wakianza kuingia ardhi ya Afghanistan ili kuikalia
Pamoja na hali hiyo na licha ya miaka 15 kupita baada ya tukio la Septemba 11, ndio kwanza wimbi la ugaidi na makundi ya kufurutu mpaka kwa ngazi tofauti vimeshadidi zaidi ya kipindi cha kabla ya hujuma hiyo. Hadi sasa makundi ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh (ISIS) na Boko Haram yanatekeleza hujuma zao katika maeneo tofauti ya dunia, ambapo hujuma zao hizo haziwezi hata kulinganishwa na zile za kundi la al-Qaidah. Katika kipindi hicho cha miaka 15, nusu ya eneo zima la Mashariki ya Kati hivi sasa inashuhudia mapigano na vita vya kubuniwa kwa lengo la kuziweka katika eneo hilo tawala vibaraka za madola hayo ya Magharibi. Mbali na hayo kiasi cha fedha ambacho kimetumiwa na Marekani na Ulaya katika kipindi hicho, kimepelekea kuibuka mgogoro mkubwa wa kiuchumi kwa madola hayo hayo ya Magharibi, mgogoro ambao umeyaweka maisha ya mamilioni ya watu duniani katika mashinikizo makubwa. Mbali na hayo kiwango cha Wamagharibi hao katika kusimamia haki za binaadamu, kimezidi kudhoofika siku hadi siku.
Askari wa Marekani pia wakilinda zao la mpopi kwa ajili ya kujitajirisha
Kupitia vita hivyo dhidi ya ugaidi ndipo kukaibuka jela zenye majina ya kutisha kama vile Abu Ghuraib na Guantanamo na kupelekea kuliweka jina la Marekani katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa utesaji na unyanyasaji mkubwa wa wafungwa. Wakati huo huo na kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi, ulimwengu ukashuhudia pia ongezeko kubwa la operesheni za ujasusi ambazo hazikuwahi kushuhudiwa katika historia ya mwanadamu zinazofanywa na Marekani kiasi kwamba hata viongozi waitifaki wa Washington nao waliandamwa na ujasusi huo. Kwa hakika tukio la Septemba 11 mwaka 2001, liliathiri uwiano baina ya uhuru na usalama, kiasi kwamba ni baada ya hapo ndipo madola hayo yakapiga teke uhuru na usalama kote duniani. Hadi sasa ni maeneo machache sana ambayo hayakabiliwi na hatari ya mashambulizi ya kigaidi, suala ambalo linaashiria kuhusika kwa Marekani katika kuasisi saratani ya ugaidi baada ya tukio la Septemba 11. Kwa msingi huo, tunaweza kusema kuwa, kile kinachotajwa kama matunda na mafanikio ya vita dhidi ya ugaidi baada ya shambulio la Septemba, ni matokeo yasiyo na tija wala faida yoyote kwa ulimwengu.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE