March 22, 2017

 

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amedaiwa kuwatishia kuwafunga jela miezi 6 au kuwapa tuhuma za dawa za kulevya bila kupitia mahakamani wafanyakazi wa kituo cha utangazaji cha Clouds kwa kukataa kurusha habari aliyoitaka.

Hayo yamebainika katika ripoti ya uchunguzi wa tukio la mkuu huyo wa mkoa kuvamia katika kituo cha utangazaji cha Clouds akiwa na askari wenye silaha, ripoti ambayo pia imependekeza mamlaka husika kumchukulia hatua za kinidhamu.
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mbele ya wanahabari katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Kamati ya uchunguzi Deodatusi Balile amesema kamati hiyo haikuweza kumpata Paul Makonda kwa ajili ya mahojiano.
Akitaja mambo yaliyobainika katika sakata hilo, Balile amesema kamati hiyo iliyohoji watu mbalimbali wakiwemo wafanyakazi 14 wa kituo cha Clouds, imejiridhisha pasipo shaka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alivamia katika kituo hicho saa 4:30 usiku wa Machi 17 akiwa anaendesha gari yenye namba za usajili T553 BFH.
Amesema uchunguzi wa kamati umebaini kuwa sababu ya uvamizi huo ni habari iliyodaiwa kumuhusu mwanamke aliyedai kuzaa na Mchungaji Josephati Gwajima ambapo alitaka habari hiyo iruke kwenye kipindi..
Pia kamati hiyo imethibitisha kuwa Makonda na askari waliingia hadi katika vyumba ambavyo hawakupaswa kuingia, na waliingia hadi kwenye studio ambayo inarusha matangazo na kutoa vitisho kwa watangazaji, waandaji na wafanyakazi wengine, kiasi cha baadhi yao kuagua vilio.
“Vitisho hivyo ni askari wenye silaha za moto, kuingia ndani ya studio kibabe wakiwa na silaha za moto, Makonda aliwatisha usiku huo kwamba angewafunga jela miezi sita, pia angewakagua watangazaji wa kipindi kama wanahusika na dawa za kulevya, au kuwabana wadhamini wa kipindi na pengine kuwaingiza kwenye orodha ya wahusika wa dawa za kulevya endapo wangeendelea na msimamo wao” Amesema Balile
Deodatusi Balile akisoma taarifa hiyo
Pia amesema kamati imebaini kuingiliwa kwa uhuru wa habari kinyume cha sheria kwa kulazimisha kutangazwa kwa habari isiyokidhi vigezo.
Kuhusu wafanyakazi kupigwa, Balile amesema kamati hiyo haikuona uthibitisho wowote kuwa kuna watu walipigwa, isipokuwa wapo waliolia kutokana na vitisho vya kupelekwa jela miezi 6.
Kamati hiyo imetoa mapendekezo manne ikiwa ni pamoja kumtaka Makonda aombe radhi kwa tasnia ya habari, kumtaka Waziri kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka yake ya uteuzi ili hatua zichukuliwe, vyombo vya dola vianzishe uchunguzi wa ndani dhidi ya askari walioingia.
Amesema kamati hiyo ilijirisha kuwa Makonda hakuwa tayari kuhojiwa wala kutumia fursa ya kujieleza jambo ambalo hata hivyo halikuathiri uchunguzi wa kamati hiyo.
"Tulianza kwa kumpigia simu, lakini hakupokea, tukaamua kumpelekea ujumbe hakuujibu, tukatumia wasaidizi, wakatutaka tufike ofisini kwake, tulifanya hivyo, tulifika lakini ilielezwa kuwa ana mgeni, ulipofika muda akatuita, tukaelekezwa kupita ngazi za mbele lakini yeye akapita mlango wa nyuma akaondoka. Tukaambiwa tumsubiri, tukasubiri lakini baadaye tukaambiwa amepata shughuli nyingine kwa hiyo hataweza kurejea ofisini". Amesema Balile
                           

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE