Rais John Magufuli amewaambia wakazi wa mji wa Bomang’ombe katika Jimbo la Hai kuwa amewasamehe.
Alitoa kauli hiyo akiwa katika jimbo hilo la Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe baada ya kuwaona baadhi ya wananchi wakiwa wameshika jani
la “Sale” ambalo hutumiwa na wenyeji kuomba msamaha.
Jani hilo linaloheshimiwa sana na wachaga wa mkoa huo, ndilo ambalo mtu
akimpelekea mtu aliyemkosea na kumuomba yaishe, anayeombwa kupitia jani
hilo hana jinsi lazima akubali.
“Nawashukuru sana wote mliokuja na haya majani ya mti. Nafahamu maana
yake na mimi nimewasamehe wote. Najua na ninyi mmenisamehe wote,”amesema
Rais Magufuli huku akishangiliwa.
Ingawa Rais Magufuli hakuweka bayana walichomkosea, lakini katika
uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, Rais Magufuli alipata kura 29,341 wakati
mpinzani wake wa karibu, Edward Lowassa akipata kura 49,125.
“Tushikamane kwa pamoja tujenge nchi yetu. Hakuna Mtanzania anayekula
vyama, Mtanzania anataka maendeleo, anataka hospitali, barabara, anataka
madawa, maji yapatikane umeme,”alisema Rais.
“Hii ndio maana niko hapa kwa ajili yenu, naomba mniamini na Serikali
yangu tuko kwa ajili ya kuijenga Hai na Tanzania kwa ujumla. Aika mae,
Aikambe (Asanteni sana),”alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kuwashukuru wakazi wa Jimbo hilo kwa
kura alizosema ni nyingi na ambazo zilimuwezesha kuwa Rais na akawaahidi
kuwa atawaletea maendeleo bila kujali vyama.
“Ninawashukuru sana nataka niwaahidi mimi nitawafanyia kazi Watanzania
wote bila kujali vyama vyao, bila kujali makabila yao, bila kujali dini
zao bila kujali hata sura zao,” alisema.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment