
Muungano wa vyama vya upinzani
nchini Kenya National Super Alliance (NASA) umemteua aliyekuwa waziri
mkuu Raila Odinga kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika
Agosti mwaka 2017.
Bw Odinga sasa atakabiliana na Rais Uhuru Kenyatta atakayetumia chama cha Jubilee kuwania muhula wa pili.
"Hii
ni heshima kubwa sana ambayo ndugu zangu wamenifanyia, kwa kuniweka
nipeperushe bendera ya NASA. Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku
nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali
tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya
mpito," alisema Bw Odinga akihutubu baada ya kutangazwa kuwa mgombea.
Amesema atakuwa kama Joshua kwenye Biblia na kuvusha Wakenya hadi nchi ya ahadi.
"Sisi
tuko kama timu, yenye pembe tano (Pentagon), wamenipa utepe wa nahodha,
hiyo inaniunganisha mimi nao na Wakenya wote, tutatembea pamoja bega
kwa bega. Tunataka kubadilisha Kenya na kutekeleza ndoto ya waanzilishi
wa taifa letu".
Alisema serikali yake itaangazia kumaliza
umasikini, kuimarisha afya, kuboresha uchumi, kubuni nafasi za kazi na
kurejesha gharama ya elimu na maisha chini.
Bw Odinga pia ameahidi kuhakikisha walimu na madaktari,pamoja na wafanyakazi wengine wanalipwa mishahara mizuri.
Kadhalika, ameahidi akishinda serikali yake itamaliza rushwa serikalini.
Makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi amesema viongozi wote wakuu
wa muungano huo wamekubalina kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.
"Tumekubali
kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka
ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya walitaka, lakini
haikuidhinishwa," amesema.
Amesema mpango wao ni kuwa wadhifa wa kinara wa mawaziri na msaidizi wake, kama ilivyokuwa kwenye rasimu hiyo ya katiba.
Mgombea
mwenza wa Bw Odinga atakuwa makamu wa rais wa zamani Bw Kalonzo
Musyoka, kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement.

Bw Musyoka alikuwa makamu wa rais serikali ya Mwai Kibaki
Waziri mkuu mratibu wa shughuli za serikali atakuwa kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi.
Naibu waziri mkuu mratibu wa uchumi atakuwa kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula.
Kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto atakuwa naibu waziri mkuu atakayesimamia utawala na huduma za jamii.

"Hatutasherehekea, na bado hatujasherehekea, hadi tuing'oe serikali
ya Jubilee kutoka madarakani. Ni mapema mno," alisema Bw Musyoka
alipokuwa anahutubu baada ya kutangazwa kwa mgombea huyo wa urais.
"Tumegundua
kwamba muhimu zaidi katika demokrasia ni kuitekeleza. Nilisema awali
kwamba niko tayari kuwa hata mtu wa kufagia katika serikali ya NASA,
mradu tu raia wa Kenya apate heshima yake. Wananchi wameamua huu ni
mwaka wa mabadiliko. Mabadiliko hayo yanaanza nanyi (raia)."
Bw Musyoka amesema muungano wa NASA utaangazia zaidi kumaliza umaskini.
Alieleza
matumaini yake kwamba mkataba wa sasa hautavunjwa, kama ilivyokuwa
awali kwa makubaliano ya kugawana mamlaka katika miungano ya awali.
Amesema muungano wa sasa umefanywa wazi na kusajili kwa Msajli wa Vyama.
Mpangilio wa Upinzani
- Raila Odinga - Mgombea urais
- Kalonzo Musyoka - Mgombea mwenza
- Musalia Mudavadi - Waziri Mkuu
- Moses Wetangula - Naibu Waziri Mkuu
- Isaac Ruto - Naibu Waziri Mkuu
Bw Odinga ni mwanasiasa anayesifika sana kwa ushawishi wake
kisiasa na amekuwa katika msitari wa mbele kuunda vyama vya miungano na
wanasiasa ambao ni mahasimu wake.

Viongozi hao awali walizindua nembo ya muungano huo
Odinga ni nani?
Baada ya
uchaguzi wa mwaka 1997 ambapo Raila alishikilia nafasi ya tatu, kufuatia
kuundwa kwa muungano wa chama chake (NDP) na chama cha rais wa zamani
Daniel moi (KANU), aliteuliwa kama waziri wa kawi katika serikali ya
muhula wa mwisho wa Moi.
Mwaka 2002, baada ya Moi kumuunga mkono
uhuru Kenyatta, kama mrithi wake, Raila na maafisa wengine wa KANU
ikiwemo Kalonzo Musyoka na wafuasi wengine, walipinga ungwaji mkono wa
Kenyatta kugombea Urais.
Waliungana na kiongozi wa upinzani Mwai
Kibaki na na kuunda muungano wa National Rainbow Coalition (Narc) ambao
baadaye ulishinda uchaguzi wa mwaka 2002.
Raila aliungana na Rais Mwai Kibaki kuunda serikali ya Muungano ya NARC baada ya kumuondoa mamlakani rais mstaafu Daniel Moi.
Mwaka
2005 aliungana na Uhuru Kenyatta aliyekuwa kama kiongozi rasmi wa
upinzani, ili kushinda kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba chini ya
serikali ya Rais Kibaki .
Wakati Kibaki alipomfuta kazi na
washirika wake, aliunda chama cha ODM ambacho kilipiga kura ya 'La'
dhidi ya rasimu ya katiba mpya ambayo ilishindwa mwaka 2005.
Aliongoza
kampeni mwaka 2007 na kwa shingo upande kukubali ushindi wa rais Kibaki
Katika uchaguzi uliokumbwa na utata, ghasia na mauaji.
Lakini hatimaye alilazimika kujiunga na Kibaki katika serikali ya Muungano.
Disemba
mwaka 2012, Raila alilazimika kupiga moyo konde na kurudiana na Kalonzo
Musyoka chini ya muungano wa CORD, kwani daima husema katika siasa,
hakuna maadui wa kudumu.
Raila anaamini kuwa Wakenya wanastahili kuhudumiwa vyema zaidi kuliko ahadi wanazopewa na kwamba chini ya utawala wake.
Raila anaahidi kuleta mageuzi na kuhakikisha uongozi bora.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment