June 14, 2017

 

KOCHA Mkuu wa timu ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga, hajawaorodhesha wachezaji wawili wa Simba, kiungo Said Ndemla na mshambuliaji Ibrahim Hajib katika kikosi chake cha wachezaji 22 alioteua kwa ajili ya Kombe la COSAFA Castlenchini Afrika Kusini baadaye mwezi huu.

Badala yake, Mayanga amemrejesha mshambulijai Elias Maguri anayecheza Oman na kuita chipukizi wapya sita ambao ni mabeki Hamim Abdulkarim kutoka Toto Africans ya Mwanza, Nurdin Chona kutoka Tanzania Prisons ya Mbeya, viungo Salmin Hoza aliyesajiliwa Azam FC kutoka Mbao FC ya Mwanza, Raphael Daudi wa Mbeya City na washambuliaji Stahmili Mbonde wa Mtibwa Sugar na Shaaban Idd Chilunda wa Azam FC. Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, inatarajiwa kuanza kambi rasmi kesho Jumapili Juni 18, mwaka huu. Kambi hiyo itakuwa kwenye Hoteli ya Urban Rose, iliyoko Mtaa wa Jamhuri katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Taifa Stars inajiandaa na michuano ya Cosafa inayotarajiwa kuanza Juni 25, mwaka huu. Michuano hiyo, inaandaliwa na Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika ambako Tanzania - mwanachama wa Cecafa, imepata mwaliko kushiriki.
Tanzania imepangwa kundi A ambako wapinzani wake ni Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland zitakuwa na mechi maalumu (play off) ili kuingia robo fainali.
Kwa mujibu wa Mayanga, kikosi hicho kinaundwa na makipa Aishi Salum Manula  (Azam FC), Benno David Kakolanya  (Yanga SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC).
Mabeki ni Shomary Salum Kapombe (Simba SC), Hassan Kessy (Yanga SC), Gadiel Michael (Azam FC), Hamim Abdulkarim (Toto Africans FC), Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Mbonde, (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons).
Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Salmin Hoza wa Mbao FC, Muzamil Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Kichuya (Simba SC).
Washambuliaji ni Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Yussuf (Azam FC), Stahmili Mbonde (Mtibwa Sugar), Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE