June 21, 2017

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Maji Mhandisi Gerson Lwenge, Balozi wa India hapa Nchini Sandeep Arya, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo pamoja na Viongozi wengine wa Mkoa wa Pwani na Serikali akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mradi Mkubwa wa Maji wa Ruvu Juu Mlandizi Mkoani Pwani.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia kabla ya kuzindua Mradi wa maji wa Ruvu juu Mlandizi mkoani Pwani.
PICHA NA IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Juni, 2017 amezindua viwanda vikubwa vitatu na mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam ikiwa ni siku yake ya pili ya ziara ya kikazi ya siku 3 mkoani Pwani.
Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amezindua kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Tanzania Ltd kilichopo katika eneo la viwanda Kibaha ambacho kina uwezo wa kutengeneza mifuko ya sandarusi 53,000 kwa siku kwa ajili ya kuhifadhia mazao.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania Bw. Joseph Otieno Wasonga kimeajiri watu 110 na kimejengwa kwa gharama ya takribani Shilingi Bilioni 8.
Pili, Mhe. Rais Magufuli amezindua mradi wa kutengeneza matrekta 2,400  aina ya Ursus ambao utagharimu Shilingi Bilioni 55, na matrekta hayo yatasambazwa nchi nzima kwa ajili ya kuboresha sekta ya kilimo.
Mradi huu unamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na utazalisha matrekta ya aina 6 zenye nguvu ya kuanzia HP50 hadi HP 85.
Tatu, Mhe. Rais Magufuli amezindua kiwanda cha chuma cha Kiluwa Steel Group kilichopo Mlandizi ambacho katika awamu hii ya kwanza kina uwezo wa kuzalisha tani 500,000 za nondo kwa mwaka na awamu ya pili kitaongeza uzalishaji hadi kufikia tani 1,200,000 kwa mwaka.
Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing amesema kiwanda hicho kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania Bw. Mohamed Said Kiluwa kwa asilimia 51 na asilimia 49 zinamilikiwa na mwekezaji kutoka China ni muendelezo wa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya China na Tanzania.
Aidha, Shirika la Reli Tanzania (TRL) limejenga njia ya reli ya kilometa 3.5 inayounganisha kiwanda hicho na reli ya kati ikiwa ni juhudi za kurahisisha usafirishaji wa malighafi na vyuma vinavyozalishwa kiwandani hapo kwenda ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika miradi hiyo, Mhe. Rais Magufuli amepongeza uwekezaji huo na ameagiza vyombo vinavyohusika kutoa vibali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hapa nchini viondoe urasimu ambao umekuwa ukiwakatisha tamaa wawekezaji kujenga viwanda.
Mhe. Dkt. Magufuli ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda hivyo kujali maslahi na usalama wa wafanyakazi waliowaajiri, amezitaka benki hapa nchini kujielekeza kufanya biashara na wananchi kwa kuwakopesha mitaji wafanyabiashara na wajasiriamali badala ya kutaka kufanya biashara na Serikali na ameiagiza Wizara ya Nishati na madini na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha viwanda vya chuma vinatumia malighafi za hapa nchini kutoka Mchuchuma na Liganga.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amezindua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu ya maji ya kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam uliojengwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 200 ikiwa ni mkopo kutoka Serikali ya India.
Kabla ya Mhe. Rais Magufuli kuzungumza na wananchi waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu wa India Mhe. Nalendra Modi ametoa salamu kwa njia ya luninga ambapo amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake kwa kufanikisha mradi huo ambao utasaidia kuondoa kero ya uhaba wa maji iliyowakabili wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwa miaka mingi na utaboresha maisha ya watu.
Katika salamu hizo zilizowasilishwa na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Sandeep Arya Mhe. Waziri Mkuu Modi ametangaza kuwa Serikali yake imepitisha kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 500 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 1 ambazo Tanzania itakopeshwa kwa ajili ya kusaidia miradi ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa India Mhe. Nalendra Modi kwa kutoa mkopo huo na amesema upanuzi wa mradi wa maji wa Ruvu Juu pamoja na mkopo huo vinaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria kati ya Tanzania na India.
Mhe. Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kujipanga vizuri kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji inayosuasua, kudhibiti upotevu na wizi wa maji na kuwakatia maji wadaiwa sugu wote.
Kesho tarehe 22 Juni, 2017 Mhe. Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya kikazi ya siku 3 Mkoani Pwani kwa kuzindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona Drink Ltd, kuzindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agric Company na kuzindua mradi wa barabara ya Bagamoyo – Msata.

Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kibaha, Pwani
21 Juni, 2017

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE