Mwanafunzi Witness Mbalinga alipokuwa akiongea na wanahabari juzi nyumbani kwao Mtwivilla |
Hapa ndipo mwanafunzi huyo anapoishi |
“KAANDIKENI
mnachoweza kuandika, ila mimi mtoto wangu hasomi shule ya kata ni bora akae
nyumbani mpaka nitakapopata ada ya kumlipia katika shule ya bweni,” haya ni
majibu ya mama mzazi wa Witness Mbalinga (13), Menciana Mbalinga aliyeyatoa kwa
wanahabari juzi.
Wanahabari
hao akiwemo mwandishi wa mtandao huu walikuwa wakifuatilia sakata la mama huyo kumzuia
binti yake huyo kujiunga katika shule ya sekondari ya Mtwivilla baada ya
kufaulu mtihani wa darasa la saba.
Tangu
wanafunzi wenzake wajiunge na elimu hiyo Januari mwaka huu, Witness aliyemaliza
shule ya msingi Mtwivilla mwaka jana na baadae kuchaguliwa kujiunga na shule ya
sekondari ya Mtwivilla anashinda nyumbani kama binti wa kazi.
Huku
akitokwa na machozi binti huyo aliwaeleza waandishi wa habari waliofanikiwa
kufika nyumbani kwao mtaa wa Mtwivilla, mjini Iringa kwa mahojiano naye kwamba;
“nina miezi mitatu sasa niko tu nyumbani, mama hataki nisome shule ya kutwa.”
Alisema
baada ya kukataliwa kujiunga katika shule hiyo ya sekondari ya Mtwivilla, mama
yake huyo alimpeleka wilayani Kilolo ambako alifanya mtihani wa kujiunga na
shule ya sekondari ya St Michael.
“Nilifanya
mtihani na nikafaulu lakini siku zinazidi kwenda na kila nikijaribu kuuliza
mama amekuwa akinizungusha,” alisema.
Witness
alisema hatma yake ya elimu iko mikononi mwa mama yake huyo aliyemuahidi
kumpeleka katika shule hiyo ya bweni leo Jumapili.
Pamoja
na kutokwa machozi, Witness aliongea kwa kujiamini huku akionesha kiu aliyonayo
ya kuendelea na masomo ya sekondari hata katika shule aliyochaguliwa kujiunga
nayo.
Wakati
akizuiwa kuendelea na masomo ya sekondari, mzazi huyo ametuhumiwa kumzuia
bintiye kwenda kwa ndugu zake kwa kile kilichoelezwa na binti huyo kwamba
hataki suala hilo la hatma yake ya shule lilete mjadala ndani ya familia.
“Nina
amini kama marehemu baba yangu angekuwa hai, ningekuwa shule kama ilivyo kwa
wanafunzi wenzangu,” alisema na kuongeza kwamba baba yake mzazi alifariki miaka
minne iliyopita.
Katika
majibu yake kuhusiana na tuhuma hiyo mama mzazi wa binti huyo alisema “kilichonikwamisha
ni fedha ya kodi ninayopata kutoka katika meza ya biashara aliyokuwa akifanyia
mume wangu katika soko kuu la mjini Iringa.”
“Pamoja
na kutolipwa, nawahakikishia jumapili hii lazima nimpeleke shule kwasababu
kuna mtu ameahidi kunikopesha,” mama huyo anayeendesha mgahawa katika jengo la
IMUCU mjini Iringa alisema.
“Mie
sina kosa kwasababu sina mpango wa kuona mtoto wangu anabaki nyumbani, yule ni
mtoto wangu na ni lazima atapata haki yake ya elimu kama watoto wangu wengine,”alisema.
Bila
kuwataja majina alisema anao shemeji na wifi zake wengi mjini Iringa ambao
mbali na kutofika nyumbani kwake kujua hali ya familia yake baaada ya mumewe
kufariki, hawana msaada wowote kwake na watoto wake.
Alipoulizwa
kwanini kama hakuwa na maandalizi ya kutosha ya kumpeleka binti yake shule ya
bweni hakumuacha aendelee na masomo katika shule hiyo aliyochaguliwa mpaka pale
ataakapokamilisha maandalizi yake?: alisema;
Nia
yake nzuri ya kumpeleka mwanae huyo katika shule ya bweni ilikwamishwa na
wadeni wake waliochelewa kumpa fedha zake kwa wakati kama walivyokuwa
wamekubaliana.
Mapema
mwaka huu, Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi alitoa agizo kwa madiwani
wote wa halmashauri hiyo kuwasaka wanafunzi ambao hawajulikani waliko baada ya
kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.
Source:seetheafrica.blogspot.com/
0 MAONI YAKO:
Post a Comment