Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya
amesema kutumia lugha ya kejeli dhidi ya mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ilikuwa mbinu ya kupata
ushindi katika majadiliano wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
Mwandosya alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari
nje ya ofisi za CCM baada ya kuhudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya
chama hicho ya Mkoa wa Mbeya.
“Katika eneo kama lile ni lazima utumie lugha ambayo ilikuwa siyo nzuri
kwa Tume ya Warioba ili kuweza kusisitiza jambo fulani au ni njia ya
ushawishi ili kuweza kupata ushindi,” alisema Mwandosya.
“Hivyo tunapaswa kuachana na maneno na maudhi yaliyofanyika wakati ule
na kufuata misingi katika kuhakikisha tunapata katiba mpya kwa masilahi
ya wananchi wetu.”
Alipoulizwa kuhusu Bunge hilo kutozingatia maoni ya wananchi kwa kuondoa
vipengele vilivyokuwa katika Rasimu ya Katiba, alisema kuwa maoni ya
wananchi yaliyotolewa, hayakuwa kura ya maoni.
Mwandosya alitetea kuwa katika vikao vya Bunge hilo hawakuwa na rasimu
yoyote ambayo waliitumia katika kutafuta Katiba Mpya, zaidi ya ile
iliyoandaliwa na Tume ya Warioba.
“Hapa naomba nifafanue vizuri kuwa hatukuwa na Rasimu yoyote ambayo
tuliitumia nje ya Rasimu ya Jaji Warioba na ndiyo hiyo itakuja kwa
wananchi kwa ajili ya kuipigia kura ya ndiyo au hapana,” alisema.
Kuhusu kuondolewa kwa vipengele ambavyo vinawapa wananchi nguvu ya
kuwawajibisha viongozi wao, Mwandosya alisema wamefuatilia katiba zote
duniani na kugundua kuwa wananchi wana haki ya kuwawajibisha wabunge
wakati wa uchaguzi mkuu. Alisema wabunge wengi wamekuwa wakishindwa
kwenye chaguzi kwa kuwajibishwa na wananchi.
Chanzo:Mwananchi
0 MAONI YAKO:
Post a Comment