Rais Jakaya Kikwete amemwagia
sifa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa hatua ambayo inaweza
kutafsiri mengi katika medani ya siasa nchini.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi
akizungumza na wabunge wa CCM kwenye Ukumbi wa White House Dodoma
jumapili, Rais Kikwete ambaye pia mwenyekiti wa chama hicho, alisema
nguvu za Lowassa pekee zinatosha kushinda uchaguzi mdogo wa kiti cha
udiwani Kata ya Makuyuni kilichoko wilayani Monduli.
Kata ya Makuyuni iko wilayani Monduli, ambako Lowassa amekuwa mbunge wake tangu mwaka 1995.
Habari za kutoka ndani ya kikao
hicho zinaeleza kuwa Rais Kikwete alitoa kauli hiyo kuhusu kampeni za
uchaguzi huo wa Makuyuni, baada ya kuwa ametoa ruksa kwa makada wa chama
hicho wanaotaka urais kuanza kujipitisha pitisha miongoni mwa wanachama
wa chama hicho. Lowassa anatajwa kuwa miongoni mwa wanaCCM wanaotaka
kumrithi Rais Kikwete kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
“Sina tatizo na pale Makuyuni,
najua muscles (misuli) za Mzee Lowassa zinatosha kutupa ushindi; au vipi
mzee?” alidokeza mmoja wa wabunge wa CCM akimnukuu Rais Kikwete.
Uchaguzi wa Udiwani Kata ya
Makuyuni unaotarajiwa kufanyika Juni 16, mwaka huu, utakuwa wa ushindani
mkali kati ya CCM na Chadema ambao historia yao kisiasa mkoani Arusha
ni ya uhasama.Kusoma zaidi bofya
Katika uchaguzi huo, unaofanyika
baada ya kifo cha Abdillah Warsama (CCM), chama hicho kitatetea nafasi
yake kwa kumsimamisha Godluck Lerunya na Chadema ni Japhet Sironga.
Mbali na Kata ya Makuyuni,
uchaguzi wa udiwani mkoani Arusha utafanyika pia katika Kata za
Kaloleni, Themi, Kimandolu na Elerai, kutokana na waliokuwa madiwani wa
kata hizo (Chadema), kufukuzwa na chama chao.
“Mnaweza kuchafuana leo, kesho
mkapata mgombea mwenye nundu nyingi na mabandeji kila mahala, halafu
mkapata shida kumnadi,” alisema.
Siyo mara ya kwanza kwa Kikwete kumsifia Lowassa kwani aliwahi kufanya hivyo mwaka jana huko Longido wakati akikabidhi ng’ombe.
Pia aliwahi kumsifia wakati wa
kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 wakati Kikwete alipomwelezea Lowassa
kama Mbunge makini na kuwaomba watu wa Monduli kumchagua tena.
Hata hivyo, alipoulizwa kama
baada ya kuruhusiwa kuanza kujipitisha kwa wanaCCM kama anataka kuwania
urais, Lowassa alijibu kupitia watu wake wa karibuni kuwa asingependa
kuzungumzia suala hilo hasa baada ya Rais kutoa kauli hiyo.
Kutangaza nia ruksa
Kutangaza nia ruksa
Rais Kikwete aliwaeleza wabunge
hao kuwa si kosa kwa watu kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi ikiwamo urais mwaka 2015.
“Wabunge na mawaziri wenye nia ya
kutangaza nia ya kugombea urais wawe huru, kwani hiyo ni haki yao,
isipokuwa wafanye kwa wema bila kukivuruga chama na kuwagawa wanaCCM
katika makundi. Sioni tatizo watu kujipitisha. Sisi sote hapa
tulijipitisha. Lakini tufanye hivyo kistaarabu bila kuvurugana.”
Aliwaagiza wabunge wa chama hicho kwenda majimboni mwao kusikiliza kero za wananchi badala ya kusubiri wakati wa uchaguzi.
Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye naye anatajwa kuwa
miongoni mwa wagombea amewataka waandishi waache kuandika kila siku
habari za urais na badala yake waandike mambo ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana baada ya kukutana na mabalozi wa nchi zinazoendelea kuhusu
Mkutano wa Smart Partnership, unaotarajiwa kufanyika nchini, Membe
alisema ni vizuri yakaandikwa mambo ya maendeleo na si kila wakati
kuandika mambo ya urais.
“Mkutano kama huu nchi kama Kenya
watauripoti vizuri na kwa undani hivyo mfanye hivyo si kila kitu urais
2015,” alisema Membe. Mkutano huo utaanza Mei 28, hadi Juni Mosi na
utajadili jinsi gani sayansi na teknolojia vinaweza kutumika kuzikwamua
kiuchumi.
Imeandikwa na Kizitto Noya, Habel Chidawali na Boniface Meena.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment