Chama cha Wananchi CUF kimekanusha taarifa zilizoenea kuwa kimejitoa
kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) CUF imesema kuwa
haikuhudhuria katika kikao cha Ukawa kilichoendelea jana kwa sababu
kwanza hawakupata taarifa na pia walikuwa na kikao cha ndani ya chama
kama katiba yao inavyotaka.
Akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam leo, Naibu Katibu Mkuu
wa CUF Bara, Magreth Sakaya alisema taarifa za wao kujitoa Ukawa ni za
uzushi. Sakaya alisema CUF haikuweza kushiriki kikao cha jana kutokana
na sababu za kikatiba ndani ya chama. “Katika chama chetu tunaendelea na
vikao, maamuzi magumu ya chama huamuliwa na vikao vya juu vya maamuzi
ndani ya chama,” alisema Sakaya.
Aliongeza kuwa Baraza Kuu la CUF litakutana Julai 25 kutoa maamuzi
ili wanaposhiriki vikao vya Ukawa wawe kitu kimoja kama chama. “Maamuzi
magumu ya chama huamuliwa na vikao vya maamuzi ndani ya chama, chama
chetu kimekuwa kikiendelea na vikao vya ndani ili kuwa na maamuzi ya
pamoja,” alisema. Ukawa jana walikuwa na kikao kilichodumu kwa takribani
saa 14 na walitoa taarifa kuwa wameafikiana juu ya mgombea wa Ukawa
hata hivyo atatangazwa baada ya siku saba.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment