October 24, 2015


Kinyang’anyiro cha urais nchini Tanzania kimewavutia jumla ya wagombea wanane, wote waking’ang’ania kumrithi Rais Jakaya Kikwete ikulu. Unawafahamu?

soma maelezo yao kwa ugupi
Anna Mghwira

Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo)

Ndiye mgombea pekee wa kike kinyang’anyiro cha urais mwaka huu na ndiye mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo. Mghwira, 56, anatoka mkoa wa Singida. Babake alikuwa diwani na kiongozi katika chama cha Tanu na baadaye CCM. Ana shahada ya uzamili katika Sheria na shahada ya kwanza katika Theolojia.

Chifu Lutalosa Yembe

Alliance for Democratic Change (ADC)

Alikuwa awali mwanachama wa Civic United Front (CUF) na mwenyekiti wake Shinyanga. Alijaribu kumuengua mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahim Lipumba, lakini akashindwa na mwishowe akatimuliwa chamani. Yeye yumo kwenye biashara ya madini na ameahidi kuimarisha mambo manne akichaguliwa rais: afya, maji, ukusanyaji wa ushuru na matumizi mema ya rasilimali. (Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi, Tanzania)

Edward Ngoyai Lowassa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

Ndiye mgombea mkuu wa upinzani kupitia Chadema kimoja kati ya vyama vinne vilivyoungana chini ya Ukawa. Lowassa, 62, anatoka mkoa wa Arusha. Alihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia 2005 hadi kujiuzulu kwake Agosti 2008. Lowassa alijaribu kuwania urais 1995 lakini akachujwa mapema. 2005 alimpigia debe Jakaya Kikwete ambaye aliposhinda, alimteua Waziri Mkuu. Alisaka tiketi ya CCM wakati huu na alipochujwa akahamia Chadema.

Fahmi Nassoro Dovutwa

United People Democratic Party (UPDP)

Ndiye mwenyekiti wa UPDP. Dovutwa, 58, alikuwa mmoja wa wawakilishi wa vyama vya kisiasa kama mjumbe Bunge la Katiba lililokuwa na vikao vyake Dodoma. Aliwania urais 2010 chini ya UPDP na akashinda asilimia 0.16 ya kura, baada ya kujiondoa dakika za mwisho.

Hashim Rungwe Spunda

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA)

Spunda aliwania urais 2010 akitumia NCCR Mageuzi lakini akapata asilimia 0.3 ya kura. Ni wakili wa Mahakama Kuu anayehudumu kibinafsi. Anatoka eneo la Ujiji, Kigoma. Spunda, 66, alikuwa mfuasi sugu wa Tanu na baadaye CCM, na alijiunga na NCCR Mageuzi 1996. Aliondoka NCCR Mageuzi 2012 na kuanzisha Chaumma. Aliwania ubunge mara mbili bila kufua dafu, 1995 jimboni Kawe na 2005 jimbo la Kinondoni.

Janken Malik Kasambala

National Reconstruction Alliance (NRA)

Kasambala ni mfanyabiashara ambaye aliwahi kuwa baharia. Akifanya kazi Uganda alizuiliwa na wanajeshi watiifu kwa Idi Amin Dada miaka mitatu kabla na kujiunga nao na kupigana dhidi ya wanajeshi wa Milton Obote akiwa Luteni. Alipanda ngazi na kuwa kapteni. Baada ya kuanza kwa siasa za vyama vingi 1992, pamoja na James Mapalala, walianzisha Civic Movement ambayo mwishowe ilibadilika na kuwa chama cha Civic United Front. Alikuwa katibu wa chama hicho mkoa wa Ilala na aliwania ubunge jimbo la Ukonga 2005 lakini akamaliza wa tano. (Picha kwa hisani ya tanzaniangovernment.blogspot.co.uk)

John Pombe Joseph Magufuli

Chama cha Mapinduzi (CCM)

Ndiye mgombea wa chama tawala na anatoka mkoa wa Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania. Magufuli, 56, amekuwa mbunge wa Chato tangu 1995 na amehudumu kama Waziri wa Ujenzi tangu 2011. Awali, alihudumu kama Waziri wa Ujenzi kati ya 2000 na 2005 baada ya kuhudumu kama waziri msaidizi wizara hiyo kuanzia 1995, Waziri wa Ardhi na Makao (2005-2008) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi (2008-2010). Ana shahada ya udaktari katika kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Machmillan Elifatio Lyimo

Tanzania Labour Party (TLP)

Anatoka eneo la Vunjo mkoani Kilimanjaro. Lyimo, 51, alijiunga na TLP 1999 na akawania ubunge Temeke bila kufanikiwa 2000. Alijaribu tena Arusha 2010 bila kufua dafu. Ameahidi kufanikisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii, akisema watu waliokuwa kwenye mfumo wa kisiasa wa sasa hawawezi kuaminiwa kutekeleza mageuzi hayo. Ana shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)

Related Posts:

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE