October 10, 2015


Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema anamkubali kwa asilimia 90 mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akisema anafaa kwa nafasi hiyo kwa kuwa ni jasiri na ana uwezo wa kupambana na ufisadi.
Kutokana na sifa hizo, amesema endapo atakabidhiwa nchi, atasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti rasilimali za nchi na hivyo kuifanya nchi ipae kwa kasi kimaendeleo.
Alisema katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, kuna wagombea urais hawawezi kukemea ufisadi wala kuzungumzia kwa kuwa wao wenyewe sio wasafi, kwa kile alichoeleza ukiwa mchafu huwezi kupata ujasiri wa kumnyooshea mtu mwingine kidole.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha runinga cha Star TV kijulikanacho kama Ajenda 2015 juzi, Dk Slaa aliyejiweka kando baada ya Chadema kupokea makada kutoka CCM wanaodaiwa si waadilifu, alisema kwa sasa anatafutwa Rais wa nchi, lakini mgombea asiyeweza kufafanua sera kwa kushindwa hata kuzungumza kwa dakika 10, hawezi kwenda kuongoza au watakaoongoza ni wasaidizi wake.
Dk Slaa alisema Chadema, chama ambacho awali kilikuwa kinapingana na ufisadi, kwa sasa hakina ajenda hiyo kutokana na kukaribisha wasio wasafi.
Alisema akiwa mpambanaji wa vitendo vya ufisadi, ambavyo vilisababisha kutishiwa kuuawa baada ya kutangaza ‘Orodha ya Mafisadi’ mwaka 2007, sasa anaungana na Dk Magufuli aliyethubutu kusema ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi, jambo linaloonesha ana dhamira ya kweli kwa kutaka kutimiza hilo kwa vitendo.
“Ukweli Magufuli ametokana na CCM na ana mapungufu kama binadamu, lakini ukilinganisha kati ya wagombea urais waliopo, yeye ana nafuu na anaonyesha dhamira ya kupigania serikali,” alisema.
Dk Slaa alisisitiza kuwa wakati huu mgombea urais yeyote anahitaji kuwa na wabunge wengi, lakini Magufuli anaonesha dhamira ya wazi kukataa ufisadi kwa kukataa kuwanadi wagombea ubunge wa chama chake, wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo.
Alisema, akiwa Chadema mwaka 2010 walimlaumu Rais Jakaya Kikwete kwa kuwanyanyua mkono wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi, lakini mwaka huu, Dk Magufuli amekataa kufanya hivyo licha ya kuwa ni wagombea kutoka chama chake.
Akizungumzia vitendo vya rushwa na ufisadi, alisema rushwa ndogo zinaathiri wananchi kwa kuwafanya waishi kwa unyonge kuliko kubwa ambazo madhara kwa wananchi wa kawaida ni kidogo. Alisema anasikitika chama chake kilichopata umaarufu kwa ajenda ya rushwa na ufisadi na kusikiliza nyimbo za hamasa kupinga masuala hayo, sasa hawasikiki tena.
“Kwa sasa chama cha ACT ndiyo kimerithi vita ya rushwa na ufisadi na kubeba ajenda kila wanapopita,” alisema.
Alisema Magufuli ameonesha kwa matendo kuwa anayozungumza yanatoka moyoni na siyo mdomoni, kutokana na kutokuogopa kukosa kura za baadhi ya watendaji wanaotuhumiwa kuwa mafisadi.
“Kama anatekeleza leo hajapewa rungu na akipewa itakuwaje, kwani haogopi kupoteza kura kwani ufisadi upo kuanzia vijijini na vitongojini, hatua hiyo ni ujasiri wa ajabu sana kwa mgombea,” alisema.
Alibainisha kuwa kampeni siyo ushabiki wala shamrashamra, bali ni kuangalia viongozi bora kwa kuzingatia sera. Alisema yeye baada ya kusikiliza mikutano na kuangalia kwenye mitandao na kuzingatia mapambano dhidi ya ufisadi, amebaini hakuna mgombea atakayepambana na ufisadi kama Magufuli.
Akizungumzia suala la wagombea wawili wa vyama vya CCM na Chadema kuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi, Slaa alisema kuna michakato inaendelea wakati huu wa kampeni, ikiwemo kupeleka watu katika mikutano na kutoa fedha.
Alisema hali hiyo imefanya iwe vigumu kupima ni nani anakubalika zaidi.
Alisema wapo wananchi wa aina tatu, kwamba wapo wanamjua wanayekwenda kumpigia kura, wengine wanafanya maamuzi kabla ya kampeni na wapo pia wanaofanya maamuzi kwa kubadilika pole pole mpaka mwisho wa kampeni.
Slaa pia alitahadharisha Watanzania kuwa Tanzania ni mama yao, ambaye hawezi kutokea mwingine, hivyo akichezewa, watu wote wataathirika na hawataweza kupata mwingine kama huyo.
Alitaka zifanyike kampeni zinazozingatia amani, kama zilivyofanyika mwaka 2010. Alisema ikiwa itatokea migogoro, hata wanaotangaza uongozi hawawezi kutawala makaburi, hivyo ni vyema kuzingatia misingi ya amani.
Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuzingatia sheria katika kusimamia uchaguzi na kuepuka kuwa sababu ya vurugu. Slaa alisema kamwe Watanzania wasikubali masuala ya kwenda Ikulu, kuleta balaa nchini bali kwa ujumla kuzingatia masuala ya kitaifa.

Related Posts:

  • Liberia imefanikiwa kutokomeza Ebola-WHOImage copyrightGettyImage captionMtu aliyenusurika ebola Shirika la afya duniani WHO, limetangaza kwua taifa la Liberia, limefanikiwa kutokomeza Ugonjwa wa Ebola kwa mara ya pili. Mei mwaka huu shirika hilo lilikuwa limetoa t… Read More
  • Lowassa awasili Mpanda kwa Chopa Chopa iliyowabeba Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania katika mwamvuli wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa pamoja na Mwenyekiti wake, Mh. Freeman Mbowe, ikitua kwenye … Read More
  • Mgombea mwenza wa UKAWA Juma Haji Duni atikisa jimboni kwa Nape Wafuasi wa Ukawa wakishangilia.   Mgombea Mwenza wa Ukawa kupitia Chadema, Juma Duni Haji...  Mgombea Mwenza wa Ukawa kupitia Chadema, Juma Duni Haji akisalimiana na mfuasi wa Ukawa wakati alipowasili katika mkutan… Read More
  • Magazetini Leo Kutoka Dar es Salaam Tanzania leo Ijumaa Septemba 4,2015 tumeingia kwenye chumba cha cha TZA kinachomiliikiwa na Millard Ayo na tayari tumeyakusanya Magazeti yote na stori zake kubwakubwa kukusogezea hapa, headlines baa… Read More
  • TBS kufanya msako mkali nchi nzima  Katibu  Mtendaji wa Taasisi ya Nishati Jadidifu (TAREA), Mhandisi Mathew Matimbwi (katikati), akiwaonesha wanahabari Dar es Salaam Umeme Nuru (Solar Power panels) ambazo hazina ubora zilizokamatwa zikiwa ka… Read More

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE