January 01, 2016


BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeanza kung’ata kwa kutumia kanuni ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa kelele na mitetemo.

Kwa sasa mtu akitaka kufanya sherehe mtaani, kupiga muziki kwa kelele, kuendesha ngoma za kukesha za nusu uchi (vigodoro) au ‘bai koko’ au kufanya ibada kwa kelele mitaani, atapaswa kulipa Sh milioni 10.

Pia, baa na kumbi za starehe za usiku zitakazopiga kelele, zitapaswa kulipa kiasi hicho.

Aidha, NEMC imesema pia kuwa wale watakaohusika na kelele za migodini za kutumia baruti, kupasua miamba zilizo zaidi ya matakwa ya sheria ya mazingira ya kelele na mitetemo, watapaswa kulipa Sh milioni tano ili kupata kibali.

NEMC imetaka watu kuheshimu kanuni za viwango vya kelele na mitetemo katika maeneo mbalimbali nchini. Imeonya kuwa watakaokiuka, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao. Kanuni hizo zimeanza kutumika mwaka jana (2015).

Mkurugenzi Mtendaji wa NEMC, Bonaventure Baya alisema hayo Dar es Salaam jana. Alisisitiza kuwa uchafuzi wa mazingira, unaosababishwa na kelele na mitetemo, umekuwa ukifanyika bila kujali sheria za nchi na sasa watashughulikia suala hilo ipasavyo.

Alisema hivi sasa kanuni za kudhibiti suala hilo, zimekamilika na zimeanza kutumika kikamilifu. Mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha kanuni na sheria, atachukuliwa hatua kali. Baya alitoa ufafanuzi kuwa yapo maeneo yenye kelele zaidi ya viwango vinavyoruhusiwa kisheria, ikiwamo maeneo ya migodini.

Alieleza kwamba kanuni zimeweka vigezo na tozo maalumu la kuanzia Sh milioni tano hadi Sh milioni 10, kulingana na eneo na aina ya kelele na mtetemo. Alisema mambo mengine ambayo kanuni zimeweka ni faini kwa kila kanuni itakayovunjwa na kusisitiza kuwa hatua hizo zitachukuliwa ipasavyo.

source:mtembezi.com

Related Posts:

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE