Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote kuwa makini
na wakuzaji Sanaa (Mapromota) au baadhi ya wanaojiita wadau wa Sanaa
ambao wamekuwa wakitumia njia za kiulaghai na utapeli katika kujipatia
faida na manufaa kupitia mgongo wa Wasanii.
Baraza linatoa angalizo hili kufuatia kuwepo kwa ongezeko la matukio
ya baadhi ya watu wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa
wakiwadanganya wasanii na kuwalaghai kwa kuwaahidi fursa mbalimbali kama
za maonesho ya ndani na nje ya nchi ambazo hata hivyo zimekuwa
zikiishia katika kuwaletea wasanii matatizo kiuchumi na kijamii.
Aidha, watu hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wa Serikali kuwatapaeli wasanii na kujipatia fedha isivyo halali.
BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwamba kabla hawajaingia
makubaliano yoyote na mtu, asasi au kampuni yoyote wawasiliane na
wanasheria au watoe taarifa Ofisi za Utamaduni za wilaya au manispaa
zilizo karibu nao ili kuhakikisha wanaepuka ulaghai na udanganyifu
kutoka kwa watu hao wasio waaminifu.
Aidha, kwa wasanii walioko Dar es Salaam BASATA linawaelekeza kufika
Ofisi zake zilizoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Slaam ili wapate
msaada wa kisheria na kujiridhisha kama makubaliano yao ni halali na ya
uhakika.
Mwisho kabisa, BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwa ujumla
kwamba, tangu Januari Mosi mwaka 2013 tasbia za muziki na filamu ni
rasmi hivyo Wasanii wote hawana budi kusajiliwa na Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) na wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
taratibu za uendeshaji wa kazi za Sanaa nchini.
Aidha, kila msanii anawajibika kuhakikisha anafanya kazi na mtu,
watu, asasi au kampuni iliyo na vibali halali vya kuendesha shughuli za
Sanaa na si vinginevyo.
Sanaa ni Kazi, Tuitunze, Kuikuza na Kuithamini
Godfrey L. Mngereza
Katibu Mtendaji – BASATA
0 MAONI YAKO:
Post a Comment