
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Ali Shein, akizungumza na Wajumbe wa Kamati Maalum ya CCM Zanzibar
Wakati zikiwa zimebaki siku 21 kabla ya
kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa marudio visiwani Zanzibar, Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimeibuka na hoja ya kutaka mgombea urais wa Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, akamatawe na kuwekwa ndani
kwa madai ya kujitangazia ushindi kinyume cha sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari katika
ofisi kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar jana, Katibu wa Idara ya
Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakar Jabu, alisema Maalim
Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, anapaswa kukamatwa na Jeshi
la Polisi na kufunguliwa mashitaka ya kujitangaza mshindi wa urais wa
visiwa hivyo baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 kabla ya
kufutwa siku tatu baadaye na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
(ZEC), Jecha Salim Jecha.
Kabla ya Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi
Oktoba 28, 2015, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari kuwa
matokeo rasmi waliyo nayo, na ambayo walikuwa wameyapata kutoka kwa
mawakal wao katika vituo vyote vya uchaguzi visiwani humo, yalionyesha
kuwa yeye anaongoza kwa kupata asilimia 52.87 ya kura zote na kumuacha
mpinzani wake, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, na hivyo akaitaka
ZEC itende uadilifu kwa kutangaza mshindi halali wa uchaguzi huo.
Hata hivyo, akizungumza jana, Jabu
alisema Maalim Seif alikiuka sheria za uchaguzi na hivyo anastahili
kukamatwa na kufunguliwa mashitka yake.
“Kitendo cha Maalim Seif kujitokeza
hadharani na kutangaza kuwa ameshinda urais Oktoba 25 mwaka uliopita
kabla ya kura kuhakikiwa na kutangazwa na ZEC ambayo ndiyo yenye dhamana
ni kinyume cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na kingeweza kuleta
mtafaruku wa kisiasa,” alisema Waride, aliyekuwa ameongozana na kiongozi
mwingine wa juu katikaa idara yake, Moderine Castico.
Aidha, alisema CCM ingependa kuona watu
wote walioshiriki kuvuruga uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 wanakamatwa na
kufunguliwa mashitaka kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Machi
20 mwaka huu.
Alieleza kuwa uchaguzi uliovurugika
umeipa hasara kubwa serikali lakini inashangaza kwamba hakuna hata
mtendaji mmoja aliyefikishwa mahakamani kwa kuhusika na kosa hilo.
Kuhusu wasiwasi wa kukwama kuundwa
serikali ya umoja wa kitaifa kama vyama vinavyoshiriki vitashindwa
kukamilisha masharti ya katiba baada ya CUF kususia uchaguzi wa marudio,
Waride alisema vyama vinavyoshiriki visidharauliwe na wala hakuna haki
ya kuvipuuza.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF,
Omar Ali Shehe, alisema Maalim Seif hana kosa alilofanya kwa madai ya
kutangaza mwelekeo wa matokeo kabla ya tume ya uchaguzi.
Alisema taarifa alizotangaza ni matokeo
yaliyokusanywa na mawakala wake katika majimbo na ndiyo kazi yao kwa
mujibu wa sheria ya uchaguzi.
“Vyombo vya sheria vinatambua hakuwa na
makosa kutangaza mwelekeo wa uchaguzi na kwamba, matokeo rasmi
hutangazwa na tume ya uchaguzi,” alisema Shehe.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi, alisema jana kuwa uchunguzi wa
jalada la Maalim Seif la kudaiwa kujitangaza mshindi umekamilika na
kukabidhiwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee
Ibrahim, tangu mwaka jana.
Mbali na jalada la Maalim Seif, pia
alisema majalada mengine ambayo hadi sasa yapo kwa DPP ni pamoja na
watendaji wa ZEC waliohusika kuvuruga uchaguzi wa Oktoba 25.
Juhudi za kumpata DPP Ibrahim Mzee Ibrahim kujua mwenendo wa majalada
aliyodai DDCI kuwa yamekamilika hazikufanikiwa baada ya simu yake kuwa
imezimwa.
Chanzo: Nipashe
0 MAONI YAKO:
Post a Comment