
Aliyekuwa
mgombea Urais wa UKAWA kupitia CHADEMA, Ndugu Edward Lowassa, Aprili 7,
2016 alifanya mazungumzo na Wanazuoni kutoka katika vyuo vikuu vya
ndani na nje ya nchi.
Katika
mazungumzo hayo, Ndugu Lowasa aligusia masuala mbalimbali ya Kitaifa
yakiwemo hali ya siasa nchini, kuachisha kazi watumishi wenye tuhuma
mbalimbali, na kile alichokiita tatizo la mfumo nchini.
Alichokifanya
Ndugu Lowassa ni kutaka kuwaaminisha Watanzania masuala yasiyo sahihi
kwa maslahi ya kisiasa, kwani ukweli ni kwamba; Mosi, Rais John Pombe
Magufuli hatafuti umaarufu, badala yake yeye na Serikali yake wanachapa
kazi ili kuwaletea maendeleo Watanzania kwa ujumla.
Pili,
kuhusu suala la mfumo, Tanzania haina tatizo la kimfumo, kwani iliyopo,
iliyowekwa tangu awali na waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Aman Karume ni imara na imekuwa
ikiboreshwa kulingana na mahitaji.
Ifahamike
hakuna mahali popote duniani ambako mfumo wa nchi unajiendesha wenyewe,
siku zote mfumo huongozwa na kuendeshwa na binadamu ambao kwa udhaifu
wa ama kibinadamu au wa kukusudia, hufanya makosa yanayohitaji
kusahihishwa kwa taratibu zilizowekwa.
Tatu,
Hakuna mtumishi aliyeachishwa au kusimamishwa kazi kwa sababu ya hali
ngumu ya uendeshaji wa Shirika lolote, isipokuwa hatua hiyo imechukuliwa
ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukaji na
matumizi mabaya ya ofisi na madaraka, ubadhirifu, uhujumu uchumi na
ufisadi.
Chama
Cha Mapinduzi kina ushahidi wa utendaji wa Ndugu Lowasa akiwa Waziri
Mkuu namna alivyoendesha zoezi la kusimamisha na kufukuza kazi na
kuwadhalilisha watumishi bila kufuata taratibu, hali hiyo ni tafauti
sana na hii ya sasa, kwani kila anayesimamishwa kazi, anasimamishwa kwa
kufuata taratibu zote, ili kuhakikisha kila mtumishi anatendewa haki ya
kusikilizwa.
Na
katika hili la kuwasimamisha kazi watumishi wa umma wanaotuhumiwa kwa
ufisadi, wizi na matumizi mabaya ya ofisi, Chama Cha Mapinduzi
kitaendelea kuunga mkono, kutokana na baadhi yao kuwa chanzo cha
shughuli za maendeleo nchini.
Kiongozi
au mwanasiasa anayemkosoa Rais Magufuli katika hatua anazozichukua hivi
sasa, ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, ni
wa kutiliwa shaka kwani kufanya hivyo ni sawa na kutetea wizi, ufisadi
na uporaji wa rasilimali za nchi.
Ndugu Christopher Ole Sendeka,
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
08/04/2016
0 MAONI YAKO:
Post a Comment