Baada ya Mwenyeki wa Yanga,
Yusuf Manji kuwafuta uanachama wanachama tisa wa klabu hiyo, beki wa
zamani wa timu hiyo, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ ameupokea kwa mikono
miwili uamuzi huo huku akikiri kuwa kitendo alichokifanya ni kosa.
Malima na wenzake nane, walienda kuchukua fomu za
kuwania uongozi ndani ya Yanga katika ofisi za Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) na kuonekana kwenda kinyume na taratibu za klabu hiyo.
Wanachama wengine waliofutwa uanachama na Manji kwa kosa
hilo ni Aaron Nyanda, Titus Kibula, Pascal Raiza, Amir Mataka, Said
Omary, Ally Chokoma na Amiri Msumi ambaye ni mwenyekiti wa matawi ya
timu hiyo.
Wote hao kwa kitendo walichofanya, wanatuhumiwa kushiriki katika mipango ya kuuhujumu uongozi uliopo madarakani.
Jembe Ulaya alisema hapingi uamuzi wa kusimamishwa kwake
na uongozi wa klabu hiyo baada ya kugundua kosa alilolifanya ila
amesisitiza kuendelea kuisapoti Yanga.
“Sikujua kuwa TFF hawapaswi kuendesha uchaguzi wa Yanga
ila ukimya wa viongozi wa Yanga ndiyo ukanifanya niende TFF nikiamini
wapo sahihi, hata hivyo nitaendelea kuiunga mkono Yanga,” alisema Jembe
Ulaya.
Kwa upande wake, Msumi amesema: “Nimesikia kuhusu
kufutwa kwangu uanachama lakini mtu mmoja hana mamlaka ya kufuta watu
uanachama kwa mujibu wa Katiba ya Yanga.
“Kama mtu ametenda kosa, anapewa barua na kuitwa kwenye
kamati kwa ajili ya kujielezea, ikishindikana anatakiwa apelekwe kwenye
mkutano mkuu akajadiliwe kwani wenye kauli ya mwisho ni wanachama.
“Pia zile sauti zinazolalamikiwa kweli ni zangu lakini
hakuna sehemu inayotaja mambo ya rushwa, naomba ieleweke hivyo. Ila
Yanga ni kitu kimoja haihitaji sababu za kufarakana.”
0 MAONI YAKO:
Post a Comment