Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
amepuuzilia mbali madai ya Washington kuwa iko tayari kufanya mazungumzo
na Iran juu ya masuala mbalimbali ya kieneo.
Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo jana jioni alipowapokea
wanafunzi wa vyuo vikuu na wakuu wa jumuya za wanachuo wa vyuo hivyo
hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina
haja na ushirikiano wa aina hiyo na Marekani na kusisitiza kuwa, lengo
kuu la Washington ni kuidhalilisha Iran na kudunisha nafasi yake katika
eneo hili.
Kadhalika Ayatullah Khamenei amekosoa vikali mwendo wa kinyonga wa kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya Vienna na kusema kuwa, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na Bunge la Kongresi la nchi hiyo zingali zinalitazama taifa la Iran kwa jicho la uadui. Makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 maarufu kwa jina la JCPOA yalianza kutekelezwa mwezi Januari mwaka huu ambapo pande hizo mbili ziliahidi kwamba zitatekeleza kivitendo mambo yaliyoainishwa kwenye makubaliano hayo.
Katika mkutano wa jana jioni na wanachuo hapa mjini Tehran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwapa fursa wanafunzi hao wa vyuo vikuu kueleza matakwa na matarajio yao sambamba na kutoa maoni kuhusu masuala kadha wa kadha ya kitaifa.
Katika hotuba yake pia Ayatullah Ali Khamenei aligusia masuala ya makubaliano ya nyuklia, uhusiano wa nchi hii na Marekani, uchumi wa kimuqawama na mustakabali wa taifa la Iran.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment