
Siku za hivi karibuni kumekuwa na mvutano mkubwa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ikumhusisha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Lipumba na viongozi wengine wa chama hicho.
Jambo kubwa linalozua mvutano ni uamuzi wa Prof. Lipumba kutaka kurejea kwenye nafasi ya ueneyekiti wa chama hicho wakati alishaandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo.
Mwezi Agosti, 2015 wakati vyama vingi vikijiandaa na uchaguzi mkuu, Prof. Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu baada ya CHADEMA, ikiwa ni moja ya vyama vinavyounda UKAWA kumteua Edward Lowassa kuwa mgombea urais kwa mwamvuli wa UKAWA. Juni 10, 2016, Prof. Lipumba alindika barua kwa Katibu mMkuu wa CUF kutegua barua yake ya kujiuzulu na kuwa atarudi na kuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Jambo hilo limezungua mgogoro na leo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Clouds Fm, Prof. Lipumba amesema kuwa aliandika barua ya kurejea kuwa mwenyekiti kwa sababu Kamati Kuu ya CUF haikuwa imeipitisha barua yake na hata Mkutano Mkuu ulipofanyika ili kuijadili barua hiyo vurugu zilitokea hivyo haikujadiliwa.
Akizungumzia kwanini ameamua kurudi, Prof. Lipumba alisema kuwa wazee na baadhi ya wanachama ndio waliomuomba arudi kwa sababu ya matatizo mbalimbali kwenye chama.
Prof. Lipumba amekituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa kilikihujumu Chama cha Wananchi (CUF) kwa kufanya vikao vya siri na Maalim Seif bila kumshirikisha yeye. Alisema kuwa, wakati wakitafuta mgombea, Maalim Seif na Freeman Mbowe walikuwa wakifanya makubaliano mbalimbali bila kumshirikisha yeye kama mwenyekiti wa chama.
Akizungumzia kusimamishwa uanachama, Prof. Lipumba alisema kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif anakihujumu chama hicho kuhakikisha kuwa kinafusa upande wa bara ili CHADEMA ibaki peke yake. Alisema kuwa, CUF ina wabunge 10 upande wa bara, lakini wabunge wawili wamefutwa uanachama, hizo ni hujuma za kuidhoofisha CUF.
“Nilifikia uamuzi wa kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa CUF kwa sababu ya kukosekama kwa umoja ndani ya chama” alisema Prof. Lipumba. Aliendelea kueleza kuwa, Maalim Seif alikuwa akiitisha vikao vya UKAWA bila kumpa taarifa na kila alipomtaka wakae kwanza kikao cha ndani cha kupata maridhiano, Maalim Seif hakutaka.
Akizungumzia masuala ya uchumi, Prof. Lipumba alisema kuwa deni la taifa linaongezeka kwa sababu ya kasi ya ukopaji imeongezeka. Rais Mkapa alivyoingia madarakani, alitumia muda mwingi kutafuta njia ili tuweze kusamehewa madeni, na ilipofika mwak 2006 tulikuwa na deni dogo la taifa lakini tatizo lilikuwa ni kuongezeka tena kwa kasi ya ukopaji baada ya kusamehewa.
Deni la taifa huongezeka kama nchi itakopa alafu fedha zile isizitumie kwenye miradi ya maendeleo. Kama fedha zikitumika vibaya, nchi haitaweza kurudisha deni lakini ikiwekeza kwenye maendeleo inaweza kupata mapato na kulipa deni, alisema Prof. Lipumba
Akijibu swali kwanini asianzishe chama kingine, Pro. Lipumba alisema kuwa yeye ni mwenyekiti halali wa CUF, kwa sababu katiba inasema hadi mamlaka iliyokuchagua itakaporidhia kujiuzulu kwako ndio utaachia nafasi, hivyo hawezi kuanzisha chama kingine wakati ni mwenyekiti wa CUF.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment