Kamishna
wa Polisi Kanda Maalum Dar Es Salaam anatoa rai kwa wakazi wa Jiji la
Dar Es salaam na wageni wanaoingia jijini wakitokea mikoani kupuuza
taarifa za sauti zinazozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa Polisi
wanawakamata ovyo watu wanaolala kwenye nyumba za kulala wageni.
Taarifa hizo za uvumi zinazoendelea kuzagaa kwenye mitandao ya
Kijamii kama WHATSAPP, TELEGRAM na pia zimechapishwa kwenye baadhi ya
magazeti kwamba Askari Polisi wanawakamata watu ovyo mchana wakiwa
kwenye nyumba za kulala wageni kwa madai ya kukamata kwa makosa ya
uzembe na uzururaji na pia kutimiza kauli ya Raisi wa Jamhuri ya
muungano wa Tanzania ‘HAPA NI KAZI TU’.
Kimsingi niwatoe hofu raia wema kuwa tunaendelea na oparesheni za
kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwemo wanaofanya biashara ya
nyumba za kulala wageni kinyume cha sheria (guest bubu), majambazi na
wahalifu wengine wa makosa mbalimbali.
Aidha taarifa za kuaminika zimebaini kuwa baadhi ya nyumba za
kulala wageni zimekuwa zikitumika kuhifadhi magenge ya wahalifu, dada
poa na kaka poa, hivyo Jeshi la Polisi tunawajibika kufuatilia na
kuwakamata wahalifu.
Niwajibu wa Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye nyumba za kulala wageni, Hoteli
,
migahawa, Vilabu vya vileo, kumbi za starehe zinazokesha na
zisizokesha na watakaobainika kuvunja sheria, hatua kali za kisheria
dhidi yao zitachukuliwa.
Sheria ya Mwenendo ya makosa ya jinai kifungu cha 60(1) (sura ya 77
iliyofanyiwa marekebisho 2002) kinampa nguvu askari kufanya ukaguzi wa
maeneo yote yaliyotajwa hapo juu na kumkamata mtu yeyote anayetiliwa
shaka akienda kinyume na utaratibu wa biashara hizo.
Sambamba na hayo nawatahadharisha wafanyabiashara wote wa nyumba za
kulala wageni wafuate taratibu za kupokea wageni kwa kuandika kwenye
vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanayotoka, na
pale watakapomtilia mashaka mteja yeyote watoe taarifa kituo chochote
cha polisi.
Pia wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wa nyumba kumi
wanawajibika kuwatambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na
kuwachukulia hatua stahiki ili kuimarisha usalama katika jiji letu la
Dar Es salaam.
DAR ES SALAAM BILA UHALIFU INAWEZEKANA, TUSHIRIKIANE KUISAFISHA JIJI LETU
S.N.SIRRO – CP
KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM
DAR ES SALAA
0 MAONI YAKO:
Post a Comment