Rais wa TPBO, Yasin Abdallah ‘Ostadh’ akitoa heshima za mwisho.
HATIMAYE aliyekuwa bondia wa ngumi za
kulipwa nchini, Thomas Mashali ‘Simba Asiyefugika’ leo amepumzishwa
kwenye nyumba yake ya milele kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar
akisindikizwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo ndugu, jamaa na
marafiki.
Mbali na hao, Mashali aliyeuawa na watu
wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatatu iliyopita huko Kimara-Bonyokwa,
Dar, amesindikizwa kwenye safari yake hiyo ya mwisho na wanasoka,
akiwemo Athuman Idd ‘Chuji’, mabondia maarufu Tanzania, Francis Cheka,
Mada Maugo, Francis Miyeyusho, Japhet Kaseba na bondia mkongwe, Rashid
Matumla.
Akizungumza na Global Digital kwenye
msiba huo, Cheka alisema kuwa amesikitishwa sana na kifo cha Mashali
ambaye kulikuwa na pambano kati yao lililokuwa linaandaliwa ambalo
lilitarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu lakini hana budi
kukubaliana na matokeo kwa sababu kila kitu kinapangwa na Mungu.
“Katika mapambano ya ngumi kwa upande wa
uzito wa juu, kiukweli Tanzania imepoteza mtu muhimu sana. Mashali
ameondoka wakati bado tasnia ya ngumi inamhitaji lakini ndiyo hivyo
tena,” alisema Cheka.
Kwa upande wa meneja aliyefanya kazi kwa
mara ya mwisho na Mashali, Sharifu Musili, alisema kuwa kifo cha
Mashali kimetokea muda ambao hakuna aliyetarajia na kulikuwa na mipango
mikubwa alikuwa anafanya juu ya bondia huyo.
“Tulikuwa tunafanya mipango Mashali
akaishi nje ya nchi (Sweden au Ujerumani). Lakini kama haitoshi alikuwa
na mapambano kadhaa ambayo alitakiwa kupambana. Moja lilikuwa tarehe 12,
mwezi huu, lingine tarehe 26, mwezi huu na mengine mwezi unaofuata.
Inasikitisha sana, nakosa hata maneno ya kuongeza,” alisema meneja huyo.
Mashali aliyeacha watoto saba, alizaliwa
mwaka 1980, ameanza masuala ya ubondia mwanzoni mwa miaka ya 90 na hadi
umauti unamkuta, alikuwa anamiliki mkanda wa dunia wa UBO.
Mikanda mingine aliyowahi kushinda ni ya Ubingwa wa WBF Afrika, Ubingwa wa IBF Afrika, Ubingwa wa TPBO Tanzania na Ubingwa wa PST Tanzania.
Mikanda mingine aliyowahi kushinda ni ya Ubingwa wa WBF Afrika, Ubingwa wa IBF Afrika, Ubingwa wa TPBO Tanzania na Ubingwa wa PST Tanzania.
Marehemu Mashali au Simba Asiyefugika
kwa upande wa viwango vya mabondia wa ngumi za kulipwa Tanzania, alikuwa
ni wa pili huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na Cheka na ya tatu
ikichukuliwa na Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’.
Stori/Picha: Boniphace Ngumije na Denis Mtima / GPL
0 MAONI YAKO:
Post a Comment