Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo - CHADEMA, Freeman Mbowe amesema hatokwenda polisi kwaajili ya mahojiano kama alivyoitwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akilitaja jina lake kwenye orodha ya pili ya watu wanaohusishwa na biashara ya dawa za kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai na Kiongozi mkuu wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni, amesema Makonda hana amri ya kumpa wito mtu kwenda polisi kwa mujibu wa sheria ya serikali za mitaa.
Amedai kuwa mkuu huyo wa mkoa ‘amenichafulia jina langu, chama, familia na upinzani.’ “Sijawahi kufanya biashara ama kutumia madawa ya kulevya wakati wowote katika maisha yangu,” amesema Mbowe.
“Mimi ni mtu mzima, ni kiongozi wa muda mrefu sijawahi kujihusisha kwa njia yoyote ama kuassociate na yeyote anayefanya biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya,” ameongeza.
Amedai kuwa licha ya kuunga mkono vita dhidi ya biashara ya madawa ya kulevya ambayo anaamini ilipaswa ianze zamani, lakini njia inayotumika ni ya hila na kinyume cha sheria.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment