Klabu ya Simba leo imeibuka na kupinga utaratibu unaotumiwa na TFF katika kushughulikia suala la pointi 3 ilizopewa kutoka klabu ya Kagera Sugar kwa kosa la kumchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi 3, huku ikiituhumu TFF kuwabeba mahasimu wao, Yanga Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara, amesema wameshangazwa na kitendo cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kupewa jukumu la kushughulikia maombi ya Kagera Sugar ya kutaka mapitio ya maamuzi ya Kamati ya Saa 72 kwani haina mamlaka hayo kwa mujibu wa utaratibu.
Manara amesisitiza kuwa lengo la TFF kulipeleka suala hilo kwenye kamati hiyo ni moja ya mbinu za kuhakikisha inaibeba Yanga katika mbio za ubingwa, na kwamba utendaji kazi wa kamati hiyo siku zote umekuwa si wa haki kwa upande wa Simba huku akikumbushia jinsi kamati hiyo ilivyoshughulikia sakata la usajili wa Ramadhani Singano 'Messi' wakati akitoka Simba kwenda Azam FC.Akizungumzia jinsi kamati hiyo ilivyoshindwa kutoa maamuzi kuhusu pointi 3 za Kagera Sugar, Manara amesema Simba imeshangazwa na kitendo cha kamati hiyo kuwaita waamuzi wote hadi mwamuzi wa akiba wa mchezo unaolalamikiwa kuwa mchezaji huyo alipata kadi ya njano kwa ajili ya mahojiano kwa gharama za TFF, lakini cha ajabu zaidi ni hatua ya kumuita hadi mchezaji mwenyewe anayedaiwa kupata kadi hiyo.
“Historically, haijawahi kutokea mchezaji aliyepewa kadi anaitwa kuhojiwa, yaani mwizi aliyeiba anaitwa kuhojiwa kama aliiba ndiyo kilichofanyika, sasa mwizi unamuita kumuhoji kama aliiba unataka akujibu nini?”. Alisema Manara
Aidha, Manara amesema Simba inapinga hatua ya kamati hiyo kulipeleka suala hilo polisi kwa kuituhumu Simba kughushi barua pepe iliyotumika kama ushahidi katika maamuzi ya awali kwa madai kuwa jeshi hilo liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo Waziri wake ni Mdau wa Yanga, na kushauri kama wanaona barua ile imeghushiwa, wanapaswa waipeleke TCRA ambako ndiko kunahusika na mitandao.
Pamoja na hayo yote amemuomba Rais Magufuli kuingilia kati jambo hilo kwa kuwa mpira wa miguu umebeba dhamana kubwa kwenye mioyo ya watu pia kuwa na nguvu kubwa kuliko siasa kabla hawajaamua kufanya maamuzi mengine kutokana na kile wanachokiita kuwa ni hujuma wanayofanyiwa na TFF.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment