April 11, 2017


DAR ES SALAAM: Basi tena! Jana Mikocheni Makumbusho jijini hapa katika eneo maalum la kuchoma maiti, mwili wa aliyekuwa kiongozi wa Jumuiya ya Freemason Afrika Mashariki, Sir Jayantilal Keshavji ‘Andy Chande’ (89) aliyefariki dunia, Aprili 7, mwaka huu jijini Nairobi Kenya, mwili wake unachomwa moto mpaka kubaki majivu.


Kwa mujibu wa taarifa za awali, mwili wa Chande utachomwa moto katika tanuru maalum lililopo Makumbusho na tukio hilo litakuwa ndiyo ibada ya maziko.


MAMIA YA WATU TOKA NJE
Uwazi lina taarifa kuwa, mamia ya wanachama wa Freemason wanaofikia 300 wako jijini hapa wakiwa wamepiga kambi kwenye mahoteli mbalimbali ya kifahari kwa lengo la kushiriki maziko ya kiongozi huyo mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.



FREEMASON MKUU YUPO DAR
Jana Uwazi lilifika makao makuu ya Freemason, Posta jijini Dar na kuzungumza na mfanyakazi mmoja ambaye alisema sehemu kubwa ya wafanyakazi wapo msibani, Oysterbay ambako ndiko kwenye makazi ya marehemu Sir Chande huku akisema, bosi mkuu wa Freemason duniani yupo Dar bila kumtaja jina.


“We jua tu msiba ni mkubwa sana, tayari mkuu wa Freemason ameshatua Dar kwa ajili ya mazishi ya bosi Chande,” alisema mfanyakazi huyo.


WATU HAWAAMINI
Kufuatia kifo hicho, baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii walionesha shaka yao au kutojua kama wanachama wa Freemason huwa na wao wanafariki dunia. Wengine walidiriki kuuliza; ‘kwani Freemason huwa wanakufa
kabisa mpaka hawajui kinachoendelea?”

DAKTARI
Kwa mujibu wa daktari aliyekuwa akimtibu marehemu  nchini Kenya, Sir Chande aliacha uongozi wa taasisi hiyo miaka kadhaa iliyopita, alifariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi ya tumbo.
KAMA NI HAPA
Kama sehemu hiyo ni ile inayojulikana na wengi kwa umaarufu wa kuchoma watu wa kabila la Baniani, ipo mahali ambapo imezungukwa na miti mirefu, kama vile miembe, mipera na mingine isiyo na matunda. Upande wa kulia, kuna nyumba mbili ndogo nyeupe.
Upande wa kushoto kuna kitu mfano wa kaburi lililosakafiwa vyema pamoja na picha ya mtu anayeonekana kuwa na umaarufu kutokana na mavazi yake. Mbele yake kuna majengo mawili makubwa yaliyofanana kidogo. Yameezekwa kwa bati juu na kuna nguzo nne kubwa zinazoshika paa hilo.
Katikati ya jengo hilo, kuna kitu cha chuma, mfano wa kitanda na hilo ndilo tanuru la kuchomea miili ya wafu, kama ilivyo mila na desturi za Wahindi.


HATUA 11 ZINAZOTUMIKA
Kwa mujibu wa chanzo chetu chenye uzoefu wa maziko ya marehemu kwa njia ya kuchoma moto miili (cremation), kuna hatua kama 11 mpaka kumaliza zoezi la kuchoma mwili moto.
HATUA YA KWANZA
Mwili wa marehemu kuingizwa ndani ya jengo, ndugu wa karibu huvunja nazi 3 katika kaburi lililo karibu kabisa na lango kuu.
HATUA YA PILI Mwili hupelekwa kwenye tanuru ambapo mchomaji hupanga kuni juu ya tanuru hilo ambalo limeundwa kama kitanda cha chuma. Kuni hupangwa kwa umahiri mkubwa katika mfano wa vyuma vya reli. Magogo makubwa manne hupangwa kushoto, kulia magharibi na mashariki ya tanuru.
HATUA YA TATU
Kabla ya kuuweka mwili katika tanuru, ndugu wa marehemu huuzungusha mwili mara nne katika tanuru hilo.
HATUA YA NNE
Mwili wa marehemu ukiwa ndani ya sanda nzuri huwekwa katikati ya kuni kichwa kikielekezwa upande wa magharibi.
HATUA YA TANO
Kabla ya uchomaji, ndugu huhakikisha kwa macho kuwa, mwili uliolazwa hapo ni kweli wa marehemu ndugu yao aliyefariki dunia.
HATUA YA SITA
Ndugu mmoja wa marehemu huchukua kipande kidogo cha kuni chembamba kilichoshika moto na kumchoma marehemu katika unyayo mara nne na kulizunguka tanuru.
HATUA YA SABA
Hatua inayofuata ni kuchukua moto kwa kutumia koleo maalum na kuuchanganya moto na mafuta ya samli ili uweze kuwaka sana.
HATUA YA NANE
Ndugu wa marehemu huchota aina fulani za mbegu na kuzirushia juu ya mwili unaoendelea kuungua wakati huo huku ndugu wakilizunguka tanuru. Kwa kawaida mwili wa marehemu huchomwa na kumalizika kabisa baada ya saa mbili au mbili na nusu na kinachotakiwa kubaki ni vipande vya mifupa.
HATUA YA TISA
Baada ya mwili kumalizika kwa kuungua, ndugu mmoja wa marehemu huchukua chungu maalum kilichojazwa maji na kukiweka katikati ya miguu, kisha hutazama upande akiyapa kisogo mabaki ya mwili.
HATUA YA KUMI
Baada ya tukio hilo, ndugu na waombolezaji wengine wote hutakiwa kuondoka eneo la tukio bila kugeuka nyuma.
HATUA YA KUMI NA MOJA
Mabaki ya mwili ambayo kwa kawaida ni vipande vya mifupa ya mwili na fuvu, vilivyochanganyika na majivu na mkaa huchukuliwa na ndugu kwenda kuyatupa baharini.
HISTORIA YA SIR ANDY CHANDE Chande alizaliwa Mombasa nchini Kenya, Mei 7, 1928, lakini wazazi wake walikuwa wakiishi Bukene mkoani Tabora. Andy Chande alijiunga na Freemason, Oktoba 25, 1954 baada ya kupita kwenye usaili mkubwa na kuianza ngazi ya chini mpaka kuwa kiongozi wa Freemason Afrika Mashariki. Wakati wa uhai wake, Chande aliandika kitabu chenye kurasa 207 kiitwacho ‘A Night in Africa-a Journey From Bukene’ (Usiku wa Afrika-Safari Kutoka Bukene). Katika kitabu hicho, alisema  imani ya maadili na thamani ya Freemason ilianza wakati wa mazungumzo yake na Messrs Campbell Ritchie na McLean mwanzoni mwa miaka ya 1950.
Alisema alianza kutambua kuwa, Freemason ipo katika misingi yake na ni sayansi ya maisha ambayo malengo yake ni kumbadilisha binadamu kiimani na kumfanya awe anavyopaswa kuwa Anasema kuwa malengo ya
Freemason yamefunikwa na mafumbo ambayo pengine ndiyo yanayoeleza utamaduni uliojificha katika utendaji kazi wake. Aliandika kuwa, binadamu ukiwa kwenye ngazi ya kwanza (first degree), kanuni inayoongoza inamtaka mtu awe mkweli na mwenye maadili ambayo hasa Freemason inalenga kuyaweka kwenye akili ili mwanachama awe mzuri. Ngazi ya pili ya utaratibu inatilia mkazo kwenye vipaji na akili kupitia sanaa na sayansi ili kutoa mchango mzuri iwezekanavyo kwenye maisha.

Anafafanua kuwa, ngazi ya tatu inampa mtu nafasi ya kutafakari uwepo wake kwa kina na kwamba kanuni zote tatu zinafahamika kama upendo wa kindugu, kujiweka huru na ukweli. Katika kitabu hicho, Sir Chande anamalizia kwa kusema:
“Roho yangu, akili yangu na nafsi yangu, vimetajirishwa na kushiriki kwangu Freemason.”
WATU MAARUFU NCHINI
Marehemu Chande, aliwahi kukiri katika chombo kimoja cha habari kwamba, wapo watu maarufu Bongo ambao nao ni wanachama wa Freemason bila kuwataja majina, lakini alisema kuwa, watu hao ni wasanii, walimu, wafanyabiashara na kada nyingine.
Kwa mujibu wa ratiba ya kifamilia iliyotolewa jana nyumbani kwa marehemu, Oysterbay,  mazishi ya Sir Andy Chande  yatafanyika leo saa 5 asubuhi katika tanuru la kuchoma moto ‘Makaburi ya Baniani’, Makumbusho jijini hapa.
Ratiba inaonesha kuwa,  kabla ya mazishi hayo ya kuuchoma mwili moto, kutakuwa na ibada ndogo sanjari na kuaga mwili wa marehemu nyumbani kwake kuanzia saa 2 asubuhi hadi 3 halafu msafara wa kuelekea kwenye kuchomwa moto utaanza saa 4.
 


 

 




0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE