Klabu ya Yanga imepigwa faini ya jumla ya shilingi milioni 5 kwa makosa
mbalimbali iliyobainika kuyafanya kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa
ligi kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika wa 2016/17 huku wachezaji
wake watatu wakisimamishwa
Adhabu
hiyo ni sehemu ya uamuzi wa adhabu mbalimbali kutoka Kamati y Saa 72
uliotangazwa leo baada ya kupitia michezo mbalimbali za ligi hiyo ambapo
kwa upande wa Yanga umezingatia kuwa klabu hiyo imekuwa ikirudia rudia
baadhi ya makosa hasa kosa la kutoingia katika vyumba vya kubadilishia
nguo. Adhabu hizo ziko kama ifuatavyo.......
Mechi namba 236 (Mbao FC 1 Vs Yanga 0):
Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh.
1,000,000 (milioni moja) kwa kupita mlango usio rasmi katika mechi hiyo
iliyofanyika Mei 20, 2017 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Pia Yanga imepigwa faini ya sh.
1,500,000 (milioni moja na laki tano) kwa kutoingia vyumbani na faini ya
sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonyesha vitendo vinavyoashiria
ushirikiana.
Katika mchezo huo pia mashabiki wa Yanga
walivunja uzio wa ndani (fence) wa upande wa Magharibi wakati wakiingia
uwanjani kusherehekea ubingwa wa timu hiyo. Hivyo, klabu ya Yanga
imeagizwa kulipa gharama za uharibifu huo uliofanywa na mashabiki wake.
Nayo klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya
sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wake kuingia uwanjani
kushangilia baada ya timu yao kupata ushindi.
Pia wachezaji Deus Kaseke, Simon Msuva
na Obrey Chirwa wa Yanga wamesimamishwa kucheza mechi za Ligi Kuu wakati
wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha Mwamuzi Ludovic
Charles katika mchezo huo dhidi ya Mbao FC, kusikilizwa na kutolewa
uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
Naye Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo huo.
Vitendo vilivyoashiria ushirikina katika mchezo wa Yanga na Mbao FC, Kirumba Mwanza
Yanga pia imejikuta ikipigwa faini nyingine kama ifuatavyo.
Mechi namba 206 (Yanga 1 Vs Toto Africans 0).
Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh.
1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati
wa mechi yake dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Mei 9, 2017 kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi namba 231 (Yanga 2 Vs Mbeya City 1).
Timu zote mbili hazikupita kwenye mlango
rasmi wakati wa kuingia uwanjani katika mechi hiyo iliyochezwa Mei 13,
2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hivyo, kila klabu imepigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kitendo hicho.
Pia klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo.
Mbali na adhabu hiyo, kamati hiyo imetangaza adhabu nyingine kama ifuatavyo
Mechi namba 225 (JKT Ruvu 0 Vs Majimaji 1).
Timu ya Majimaji haikuingia vyumbani
wakati wa mapumziko katika mechi hiyo iliyofanyika Mei 13, 2017 katika
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na hivyo klabu hiyo imepigwa faini ya
sh. 1,000,000 (milioni moja).
Mechi namba 230 (Kagera Sugar 2 Vs Mbao FC 0).
Klabu ya Mbao imepigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa
mechi hiyo iliyochezwa Mei 13, 2017 katika Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment