Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka
Hospitali ya Aga Khan, Mustapha Bapumia (62) ameieleza Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anashangaa mtu mwenye umri mdogo kama Yusufali
Manji (41) kuwa na vyuma vinne kwenye moyo.
Alieleza kuwa na vyuma vinne kwenye moyo ni hatari na kwamba anatembea katika kamba nyembamba.
“Kitaaluma huyu ni lazima ajiangalie sana yupo katika hatari anaweza kupoteza maisha muda wowote.”
Dk Bapumia ambaye ni shahidi wa tatu wa upande wa utetezi
alimeeleza hayo leo Jumatatu mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha
wakati akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili Manji ya kutumia dawa za
kulevya aina ya Heroine.
Akiongozwa na Wakili Hajra
Mungula kutoa ushahidi, Dk Bapumia amesema yeye kwa siku huwa anawaona
wagonjwa 50 hadi 60 na kwamba Februari 21, 2017 ilikuwa ni mara ya
kwanza Manji kupelekwa kwao akiwa na maumivu ya moyo.
Ameeleza
kuwa wana utaratibu wa wagonjwa tete kuwapeleka katika kitengo cha
dharura na kwamba Manji walimpokea, wakamlaza, wakamchunguza na kuona
ana tatizo sugu la moyo pamoja na kuwa na umri mdogo.
"Nikatafuatilia
historia na kubaini licha ya kuzibuliwa kwa mishipa yake mitatu India,
Dubai na Marekani, ilikuwa bado haijaziba lakini alikuwa bado anapata
maumivu ya moyo," ameeleza shahidi huyo.
Ameeleza kuwa
walimfanyia vipimo na vilionyesha tatizo lipo na kuna sehemu ya nne
inahitaji kuzibuliwa na kwamba mgonjwa alikuwa wazi kuwa anatumia sigara
na pombe.
Kutokana na hali hiyo ameeleza walimshauri
mgonjwa ili waweze kuzibuliwa lakini akawaambia waache na akaomba dawa
kwa kuwa familia yake ipo Marekani na matibabu yake mengi yanafanyika
huko.
Shahidi huyo alieleza kuwa wao kama hospitali
hawezi kufanya chochote bila ridhaa ya mgonjwa hivyo wakampatia dawa na
akaruhusiwa Februari 24, 2017.
Alieleza kuwa siku hiyo
hiyo alirejeshwa tena hospitalini hapo nyakati za saa mbili usiku
akisumbuliwa na maumivu kwenye moyo, wakamlaza mpaka tarehe Machi 14,
2017 ambapo aliruhusiwa.
“Katika kipindi hicho Manji aliridhia na kuzibuliwa vyuma kwenye moyo.”
Ameeleza
kuwa walimpatia dawa ikiwamo za kupunguza kolestro (mafuta) kupunguza
maumivu sugu ya mgongo pamoja na kupunguza hofu ambazo zimo ndani ya
Morphine na Benzodiazepines.
Kwa upande wake Manji akijitetea aliiomba Mahakama imuachie huru.
Akitoa
ushahidi wake alieleza kuwa yeye ana matatizo ya moyo ya kurithi kutoka
kwa babu zake ambao walikwishafariki kwa ugonjwa huo.
Ameeleza
kuwa ugonjwa wa moyo ulimuanza akiwa na umri wa miaka 26 na kwamba mara
nyingi amekuwa akitibiwa nje ya nchi ikiwamo India na Marekani na ana
vyuma vitano kwenye moyo.
Akitoa ushahidi mahakamani
hapo, Manji ameeleza kuwa kila baada ya miaka miwili anavibadilisha na
kufanya uchunguzi vinafanya kazi vipi.
Akiongozwa na
wakili wake, Hajra Mungula, Manji ameeleza kuwa katika ripoti zake za
kati ya 2009 na 2016 haijawahi kutokea akaonekana kama anatumia dawa za
kulevya.
Manji akiendelea kujitetea ameeleza kuwa anatumia vidonge 30 hadi 35 kwa siku.
Manji
ameeleza kuwa polisi walikuwa wastaarabu wanampatia dawa na kwa upande
wa Magereza vidonge vilikuwa katika kabati wanampatia.
Manji
ameeleza kuwa Februari 8, 2017 alipata taarifa ya kutuhumiwa utumiaji
wa dawa za kulevya na kuripoti kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum
(ZCO).
Baada ya kuipata taarifa hiyo ameeleza aliitisha
mkutano na waandishi wa habari kukanusha taarifa hiyo na Februari 9,
2017 alikwenda polisi kwa sababu anaheshimu jamuhuri na alitaka kazi
ifanyike kwa haraka.
Ameeleza alivyokwenda alichukuliwa
na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo alikutana na
Gwajima(Askofu Josephat) na akatoa sampuli ya mkojo.
Ameeleza kuwa baada ya hapo walikwenda kukagua nyumbani kwake walichukua kompyuta, credit card na visa card.
Amesema
kuwa anashangaa kwanini walichukua hivyo vitu wakati havihusiani na
kesi ya dawa za kulevya na kuliacha sanduku lililokuwa na sindano na
vifaa tiba.
Aliongeza kuwa inajulikana kuwa kuna ugomvi
wa kibiashara ambapo wanagombea kampuni ya Tigo na kwamba hiyo kesi ni
propaganda na ni mchezo mchafu.
Amesema hiyo kesi imemuathiri yeye binafsi na baba yake alimuachia vitu viwili jina zuri na maadili kwa jamii.
Pia
imemuaribia jina kwa jamii yake, msikitini anashindwa kwenda kusali,
biashara pia na imeumiza watoto na imemfanya aachie Uenyekiti wa Klabu
ya Yanga.
Amesema kuwa kutokana na kesi hiyo anaona
aibu kukaa na viongozi ambao anafahamiana nao akiwamo Raila Odinga na
rais mstaafu Benjamin Mkapa
Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo itakapoendelea kwa ushahidi wa upande wa utetezi.
Awali
Manji alidai kuwa yeye ni mshauri wa kampuni za familia na kwamba
alikataa tuhuma za dawa za kulevya ili mahakama imsikilize na kutenda
haki na kwamba dawa aina ya Morphine na Benzodiazepines ni sehemu ya
dawa zake ambazo anatumia.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment