Daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa
ya binadamu na vifo vyenye kutia shaka, Innocent Mosha kutoka Hospitali
ya Taifa Muhimbili ameieleza Mahakama Kuu alichobaini baada ya kuufanyia
uchunguzi mwili wa msanii wa fani ya uigizaji wa filamu nchini, Steven
Kanumba.
Dk Mosha ambaye ni shahidi wa nne wa
upande wa mashtaka katika kesi ya kuua bila ya kukusudia inayomkabili
msanii wa fani hiyo, Elizabeth Michael maarufu Lulu amesema walipofungua
fuvu walibaini ubongo wa Kanumba ulikuwa umevimba.
Lulu anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake leo Jumatatu Oktoba
23,2017, Dk Mosha akiongozwa na Wakili wa Serikali, Faraja George mbele
ya Jaji wa Mahakama Kuu, Samu Rumanyika ameeleza akiwa kazini alipewa
maagizo kuwa anatakiwa kuufanyia uchunguzi mwili uliokuwa umehifadhiwa
katika Hospitali ya Muhimbili.
Shahidi huyo amesema katika uchunguzi wa
mwili wa Kanumba alibaini kuwepo uvimbe sehemu ya nyuma kwenye ubongo na
walipofungua fuvu walibaini ubongo ulikuwa umevimba.
Dk Mosha alipoulizwa na wakili wa
mshtakiwa Peter Kibatala juu ya sampuli walizopeleka kwa Mkemia Mkuu wa
Serikali kuhusu hali ya kilevi katika mwili wa Kanumba, amesema hakuwahi
kufahamu matokeo ya uchunguzi.
Pia, amesema hafahamu kama Kanumba alijigonga ukutani kwa kuwa hakuwepo eneo la tukio.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment