December 09, 2017

Msanii wa muziki Bongo, Afande Sele amemvaa vikali msanii mwenzie, Mrisho Mpoto kufuatia madai kuwa alihusika kutoa baadhi ya wasanii katika wimbo maalum uliotungwa kwa ajili ya uzalendo na kumuweka Christian Bella wakati si raia wa Tanzania.
Afande Sele amedai kitendo hicho ni kuwakosea heshima wasanii wa Tanzania na Watanzania wenyewe. Kupitia ukurasa wake wa Instagram Afande ameandika;
Rafiki yangu mkubwa mjomba mpoto kama ni kweli wewe ndio ulikua kinara ktk kusimamia utayarishaji wa wimbo maalumu wa kuhamasisha uzalendo kwa taifa halafu ukashawishi kuondolewa kwa baadhi ya wasanii wazawa ndani ya wimbo huo na badala yake ukampa nafasi rafiki yetu christian bella kushiriki ktk wimbo huo unaowahusu watanzania wkt ukijua wazi kuwa bella pamoja na ukweli ni rafiki yetu sana lkn bado yeye sio mtz bali ni mcongoman….
ktk hili mjomba umetukosea sana watanzania wenzako na kwa hakika kama ingekua kitendo chako hicho umekifanya kwa nchi zilizoshiba uzalendo na zisizovaa joho la unafki mjomba ulistahili kukatwa nywele zako na kupigwa risasi angalau tano kichwani kwa uchache tena hadharani kwani ulichofanya ni usaliti kwa nchi yako na ni aina flani ya uhaini
Baada ya kauli hiyo ya Afande Sele ilichukua saa moja tu kwa Mrisho Mpoto kujibu madai hayo, huku akieleza zaidi kushangazwa na kauli ya kupigwa risasi. Kupitia ukurasa wake wa Instagram Mrisho Mpoto alijibu.
Kaka yangu @afandeseleking Bado narudia kusema kwamba heshima nnayokupa inatoka Mbali sana kwenye chumba cha nne cha moyo Wangu… Sihitaji kupoteza wino Mwingi kukukumbusha tofauti iliyopo kati ya UZALENDO, UZAWA na URAIA kwasababu nina uhakika unazifahamu vyema isipokuwa huenda leo haujaamkia ule ubavu sahihi na ule wa ukarimu wako ulionao siku zote, mpaka ukakataa uwepo wangu hapa Duniani Kwa kunichagulia adhabu ya kupigwa risasi tano tena za kichwa… kwakua hukuniuliza hili jambo kabla Itoshe kusema hunitaki tena…hivyo basi kabla sijapigwa hizo risasi tano nitakachofanya ni kukupa maelezo machache yatakayokufanya uipate picha ya UZALENDO..
Hivi unajua kama John Okello alipigania uhuru wa Zanzibar!? Majeshi yetu yamepigania uhuru wa msumbiji na hata Chegu sio mcuba na alipigania uhuru wa Cuba na Congo pia.. Na je unajua kama kuna wazawa wanaoangamiza maslahi ya nchi na kuna wazalendo wasiobagua!? Kaka, Afrika ni moja na waafrika wote ni ndugu zetu ( umajumui Afrika, tena ukichimba huko sana kwa hapa nchini utakuna na Prof Shivji) .. na ndio maana hata mwenge wa uhuru uliwekwa juu ya mlima kilimanjaro ili kumulikia nchi nyingine.. Kumbuka hiyo mitizamo ya KIUZAWA Mwalimu aliita mitizamo membamba.. kwa maana ya kwamba ipo kwa ajili ya Kuiangamiza afrika
Na mwisho ningependa kukuuliza—>Je umezisikia shangwe za wazalendo na wazawa leo hapa dodoma baada ya kusikia Babu Seya na familia yake wamepewa msamaha wa rais!!? Wewe ni RASTA kaka.. kumbuka siku zote CHUKI HUMUUMIZA ANAYEIHIFADHI.. #AfrikaUnite
Hii si mara ya kwanza kwa wasanii hawa kurushiana maneno mtandaoni, utakumbuka hivi karibuni wakati msanii wa filamu Elizabeth Michael ‘Lulu’ alipohukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kufuatia kumuua bila kukusudia msanii Steven Kanumba, Afande Sele aliibuka na kueleza kuwa Kanumba ndiye aliyekuwa na kosa hasa kwa kutembea na mtoto mdogo kitu kilichomfanya hata yeye kususia mazishi ya msanii huyo, hata hivyo Mpoto alikuja kumkosoa Afande kwa kauli hiyo.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE