Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo
amezindua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Arusha mjini katika eneo la
Njiro kontena. Shughuli ambayo ilihidhuriwa na mamia ya wakazi wa jiji
hilo.
Akizungumza na wananchi hao Gambo alisema, “Nina
furaha sana kushuhudia tukio hili litakaloacha alama katika maisha ya
watu wetu wa Arusha,kwani wakati wa kampeni Mhe Rais Magufuli aliahidi
na tunatekeleza kwa vitendo.”
Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia
wakazi zaidi ya laki nne kutoka wilayani humo na maeneo ya jirani ili
kupunguza idadi ya wagonjwa wanasababisha hospitali ya mkoa ya Mount
Meru kuelemewa.
Vile vile Gambo anasema kwa sasa
mapato yanayokusanywa na Jiji la Arusha kwa mwaka bado hayatoshelezi
hata kulipa mishahara ya watumishi wake na kwa maana hiyo ni muhimu
kuweka mifumo thabiti ya ukusanyaji wa mapato jijini humo.
“Jiji la Arusha mapato yake ya
ndani kwa mwaka hayazidi bilioni 12 na mishahara pekee ya watumishi wa
halmashauri ni zaidi ya bilioni 40, sasa hapo ukilipa tu mishahara hela
yote inakwisha na bado unakua na deni, sasa hata fedha za maendeleo
zitatoka wapi zaidi ya kutegemea hela zinazoletwa na Magufuli??,” alihoji Gambo.
Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya
Arusha kwa awamu ya kwanza unafanyika katika moja ya maeneo ya wazi
yaliyo kuwa yakimilikiwa kinyemelela na baadhi ya wajanja wachache na
kwa sasa ujenzi umeanza ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 500
hii ikiwa ni jengo la Ghorofa moja kwa ajili ya wagonjwa wa nje.
Naye mkurugenzi wa Jiji la Arusha
Athuman Kihamia alimshukuru Gambo kwa kuweza kulipigania eneo hilo mpaka
limeweza kurudi kwenye mikono ya wananchi.
“Kwakweli kama sio jitihada zako
eneo hili lilishaondoka mikononi mwetu hivyo kwa niaba ya wananchi wa
Arusha ninakushukuru sana, pia nikuahidi tutazingatia ushauri wako wa
kulitumia eneo hili vizuri kwa kujenga majengo ya ghorofa kuanzia tano
ili kulitumia eneo hili vizuri,” alisema Kihamia.
Ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa
kukamilika mwezi Juni 2018 ambapo zaidi ya wakazi laki 4 watapata huduma
ya afya karibu na makazi yao tofauti na ilivyo.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment