Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia wasichana
wawili kwa kosa la kujihusisha na upangaji njama wa wizi wa pikipiki.
Wakati
akizungumza na wanahabari jana Disemba 23, 2017 jijini Dar es Salaam,
Kamishna wa Kanda hiyo, SACP Lazro Mambosasa amesema wasichana hao
wanaofahamika kwa majina ya Fatuma Jumanne (19) na Nasra Bakari (19),
hutumika kama chambo kukodisha pikipiki kisha kuzipeleka kwa wakabaji.
“Watuhumiwa
hawa walikamatwa baada ya askari kupokea taarifa ya tukio la
unyang’anyi huko Ukonga Mazizini ambapo Mussa Hosea dereva wa bodaboda
alikodiwa na wasichana hao kwa lengo la kuwapeleka mazizini, na wakati
wanatoa pesa walijitokeza vijana watatu na kumkaba dereva wa pikipiki na
kisha kutoroka nayo huku wasichana hao wakitoroka eneo hilo katika
mazingira yasiyo eleweka,” amesema.
SACP
Mambosasa amesema polisi walipowahoji wasichana hao, walionyesha nyumba
ilikofichwa pikipiki hiyo, huko Ukonga Mazizini kwa Kapteni Mstaafu wa
JWTZ Egno Paul (66).
Katika
tukio lingine, SACP Mambosasa amesema mnamo Novemba 11 mwaka huu maeneo
ya Vijibweni na Mbagala Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata walinzi
watatu wa kampuni ya Supreme International Guard waliokuwa zamu siku ya
tukio la wizi wa mashine ya boti HP 85 Yamaha mali ya Wizara ya Mifugo
na uvuvi yenye thamani ya milioni 18, iliyokuwa imeegeshwa kwenye ofisi
ya TAFICO Kigamboni.
“Watuhumiwa
hao baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika na tukio hilo na kwamba mashine
hiyo wameiuza Ilala kwa Bwana Katanga kwa bei ya Tsh milioni 2.5.
Katanga alipokamatwa alieleza kuwa boti hiyo imesafirishwa kwenda Kigoma
na ndipo yakafanyika mawasiliano na mashine hiyo kurudishwa jijini Dar
es Salaam,” amesema.
Amewataja
watuhumiwa hao kuwa ni, Ramadhan Omary (41), Mohamed Abdallah (40),
Rahis Faiya (29) na Mikidadi Hussein (40). Amesema upelelezi kwa
watuhumiwa wote unaendelea na ukimaliza watapelekwa mahakamani kwa hatua
za kisheria zaidi.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment