Azam FC
UONGOZI
wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo umeandika
barua rasmi kwenda Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) inayoelekea
kutokuwa na imani na mwamuzi Israel Nkongo.
Mwamuzi huyo ndiye amepangwa kuchezesha mchezo ujao wa Azam FC dhidi
ya Yanga, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex keshokutwa Jumamosi saa
10.00 jioni.
“Kama klabu, itakumbukwa kuwa mechi zetu ambazo mwamuzi huyu (Nkongo)
amekuwa akizichezesha zimekuwa na malalamiko mengi na utata mwingi juu
ya maamuzi ya uwanjani,” ilisema moja ya nukuu kwenye barua hiyo.
Barua hiyo ilizidi kueleza kuwa moja ya sababu nyingine ya
kumlalamikia mwamuzi huyo na kukosa imani naye, ni kitendo chake cha
kuzua utata mkubwa kwenye mchezo aliochezesha mkoani Mbeya wiki moja
iliyopita kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City kutokana na uamuzi
wake.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyeandika barua hiyo
na kutuma nakala kwa Kamati ya Waamuzi, TFF na Yanga, ameweka wazi kuwa
kwa kuzingatia uzito wa mchezo huo wameiomba bodi hiyo kubadilisha
mwamuzi kwa kumpanga mwingine.
Aidha katika barua hiyo, Mohamed ameongeza kuwa kutokana na timu zote
mbili kutoka katika mkoa wa Dar es Salaam, ameiomba bodi hiyo kumpanga
mwamuzi ambaye atatoka nje ya mkoa huo.
Mbali na Nkongo kupangwa kuchezesha mchezo huo, waamuzi wengine
waliopangwa kushirikiana naye ni Josephat Bulali atakayekuwa mwamuzi
msaidizi namba moja, msaidizi namba mbili atakuwa Soud Lila, mwamuzi wa
akiba ni Elly Sasii huku Omar Abdulkadir akiwa Kamishna wa mchezo huo,
wote wakitoka Dar es Salaam.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment