Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amesisitiza kuwa
ataapishwa, kutwaa madaraka na kuunda baraza lake la mawaziri hata kama
ikimlazimu kufanya hivyo akiwa mafichoni.
Katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, Bw.
Odinga amefuta uwezekano wa kufanya mazungumzo na rais aliyepo mamlakani
Uhuru Kenyatta ili kuweza kupatikana kwa suluhu ya kisiasa kati ya
wawili hao.
Bw. Odinga amesema kuapishwa kwake kutafanyika Januari 30 kama
ilivyopangwa awali na kila mkenya amealikwa kuhudhuria hafla hiyo na
kueleza kuwa huenda ikamlazimu afanye hivyo akiwa mafichoni.
Rais Kenyatta kwa upande wake amekuwa akiuhimiza upinzani wa NASA
kuachana na siasa kwani kipindi cha siasa tayari kimekamilika kwa mujibu
wa kalenda ya matukio nchini Kenya.
Matamshi ya Bw. Odinga kuwa ataapishwa na kuwa rais wa wananchi yamekuwa
yakiibua hisia mbali mbali miongoni mwa wakenya wengi wakijiuliza kule
anapoelekea kutekeleza majukumu ya urais wakati ikulu ya Kenya ina
mwenyeji ambaye ni Uhuru Kenyatta, Odinga hakubaliani na hilo.
Wachambuzi wa siasa za Kenya wamekuwa wakitofautiana kwa kauli kuwa
huenda Odinga na vinara wenzake wanatumia kisingizio cha kuapishwa kama
chambo cha kutaka mazungumzo na Bw. Kenyatta na vile vile kujumuishwa
katika serikali, lakini Bw. Odinga anasema hilo si kweli hata kidogo.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment