RPC Ahmed Msangi
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewaonya watumiaji wa mitandao ya
kijamii wanaotumia vibaya mitandao hiyo kwa kufanya uhalifu ikiwemo
kuhamasisha maandamano yasiyo halali kuwa kitendo hicho ni kosa
kisheria.
Onyo hilo limetolewa jana Machi 24, 2018 na Kamanda wa Polisi mkoa wa
Mwanza Naibu Kamishina, Ahmed Msangi wakati akizungumza na askari
waliokuwa kwenye mazoezi mbalimbali yaliyofanyika katika uwanja wa
polisi Mabatini mjini humo.
“Nafikiri wote sasa hivi mnafahamu kuna hii mitandao ya kijamii kuna watu wanapeana vihabari vya kwenye mitandao ya kijamii wafanye uhalifu, na uhalifu wenyewe ni wa kufanya maandamano au mkutano usiokuwa na taarifa, na kiukweli umepigwa marufuku,“ameeleza Kamanda Msangi na kufafanua.
“Kuna watu wanafanya fanya hayo kushawishiana, tufanye upelelezi, tuchunguze. Yeyote atayefanya hayo kushawishi tukimng’amua tuweze kumkamata. Tumkamate na tuweze kumhoji wana sababu na nia gani?” amesema Kamanda Msangi.
Hata hivyo, Kamanda Msangi amewaasa wananchi wanaotumia mitandao hiyo vibaya kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kauli hiyo inakuja katika kipindi ambacho kwenye mitandao ya kijamii kuna taarifa za watu kupanga maandamano siku ya 26 April , kitu ambacho serikali imesema maandamano hayo yapo kinyume na sheria.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment