
Mohammad Javad Zarif
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali mauaji ya wanachama sita
wa Harakati ya Mapambano ya Lebanon Hizbullah yaliyofanywa na utawala
haramu wa Kizayuni. Akizungumza na televisheni ya Press mapema leo,
Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Tehran
inalaani vikali vitendo vyote vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni wa
Israel vikiwemo vile vinavyotekelezwa na utawala huo dhidi ya watu wa
Lebanon na Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya nchi hiyo. Zarif
amesema sera ya ugaidi wa kiserikali ni sera inayofahamika ya utawala wa
Kizayuni wa Israel. Harakati ya Mapambano ya Lebanon Hizbullah
imethibitisha kuuliwa wapiganaji wake sita katika shambulio jipya la
anga lililofanywa na Israel katika mji wa kistratejia wa Quneira kusini
magharibi mwa Syria. Hizbullah imewataja wanachama wake waliouliwa jana
na Israel kuwa ni Jihad Mughniya mwana wa kiume wa Imad Mughniya kamanda
wa ngazi ya juu wa harakati hiyo aliyeuliwa kigaidi na Israel na
wapiganaji wengine watano waliotajwa kwa majina ya Mohammad Issa
aliyekuwa na miaka 42, Abbas Ibrahim Hijazi miaka 35, Mohammad Ali Hasan
Abu al Hassan miaka 29, Ghazi Ali Dawi miaka 26 na Ali Hasan Ibrahim
miaka 21.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment