January 26, 2015

 
MAMLAKA ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imefungia mabasi mawili ya Kampuni ya Ibra Line Limited, yanayofanya safari za Dar es Salaam-Arusha na Moshi-Arusha, kwa kutoza nauli zaidi, kuongeza na kufupisha ruti kinyemela.
Mabasi hayo; T 288 CBV linalosafirisha abiria kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam na T 843 BVF linalofanya safari zake kati ya Moshi na Arusha, yamezuiwa kusafirisha abiria kwa siku 30, kuanzia leo.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Meneja Leseni wa Sumatra, Leo Ngowi, alisema adhabu hiyo ni fundisho kwa wamiliki na wafanyakazi wa mabasi yenye leseni ya kusafirisha abiria, wanaokiuka masharti ya leseni hiyo kwa visingizio mbalimbali.
Kwa mujibu wa Ngowi, ukaguzi uliofanywa na maofisa wa mamlaka hiyo, kwa ushirikiano na polisi katika Kituo Kikuu cha Mabasi mjini Moshi, Januari 7, mwaka huu, umebaini kuwa, basi namba T288 CBV lilikatisha ruti na kuanzia safari yake ya siku hiyo mjini Moshi badala ya Arusha kwenda Dar es Salaam.
“Kwa maana hiyo, basi hilo liliwanyima haki ya kusafiri abiria waliokuwa Arusha wakitaka usafiri wa kwenda Dar es Salaam. Pia, wahusika katika basi hilo waliwatoza abiria nauli ya Sh 35,000 kutoka Moshi kwenda Dar es Salaam, badala ya Sh 28,500 kwa njia hiyo,” Ngowi alisema na kueleza kuwa hayo ni makosa yanayostahili adhabu iliyotolewa.
Mbali na makosa hayo, Ngowi alisema kuwa, wahusika katika basi hilo, waliandika taarifa za uongo kwenye tiketi walizowapa abiria kuwa wamewatoza nauli ya Sh 28,500 iliyoidhinishwa na Sumatra wakati waliwatoza Sh 7,000 zaidi ya iliyopangwa na mamlaka hiyo.
“Abiria waliokuwa katika mabasi yote mawili, walibughudhiwa kwa kutolewa lugha chafu siku hiyo, ambapo walitoa ushirikiano kwa kuwafahamisha ukweli maofisa waliokuwa wakifanya ukaguzi kituoni hapo, jambo lililosababisha wahusika watuhumiwe chini ya kifungu namba 18 (1) (a), cha masharti ya leseni ya usafirishaji abiria ya mwaka 2007,” alisema.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE