HALMASHAURI ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga imewaonya walimu wa shule
za msingi wanaopuuza agizo la serikali la kuzuia kuwarudisha nyumbani
wanafuzi ambao wazazi wao wanashindwa kuwalipia michango mbalimbali
ambayo imezuiwa na serikali
Kauli
hiyo imetolewa na afisa elimu wa shule za msingi katika halmashauri ya
mji wa Kahama Bw. Aruko Lukolela baada ya kuwepo malalamiko ya wazazi
katika shule za msingi za Nyasubi na Mbulu ambako imedaiwa baadhi ya
wanafunzi kurudishwa nyumbani kwa kukosa fedha hizo.
Amesema hakuna utaratibu wa kiserikali wa kumrudisha mwanafunzi
nyumbani kwa kukosa michango kwa kuwa serikali ilikwisha futa michango
yote kwenye shule za msingi na elimu hiyo hutolewa bure nchini.
Amewataka walimu wanaowachangisha wanafunzi kuacha mara moja na
atakaebainika kuendelea kuwachangisha wazazi atachukuliwa hatua za
kisheria , wakiwemo wanaodai fedha wakati wa kuwaandikisha watoto darasa
la kwanza au awali kwa kuwa wanatakiwa kuandikishwa bure.
Awali mmoja wa wadau wa elimu wilayani Kahama Bw. Joseph Chimakaguli
amesema walimu hao wamekuwa wakifanya biashara ya Fulana (T-Shirts)
ambazo madukani huuzwa shilingi elfu moja na mia tano lakini wao
wamekuwa wakiwauzia wazazi kwa shilingi elfu saba kwa fulana hali ambayo
amedai inastahili kuachwa kwa walezi na wazazi wenyewe kununua
madukani.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment