March 26, 2015


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge limepitisha muswada mchungu kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari baada ya kupitisha Muswada wa Takwimu wa Mwaka 2013, ambao pamoja na mambo mengine unataka mwandishi atakayefanya makosa kwenye kuripoti taarifa za takwimu atafungwa jela miaka miwili ama kutozwa faini ya Sh. milioni 10.

Bunge limepitisha muswada huo unaowabana waandishi wa habari siku chache kabla ya kuwasilisha miswada mingine miwili Jumanne ijayo siku ambayo Serikali inatarajiwa kuwasilisha muswada wa Sheria ya kupata Habari wa Mwaka 2015 na ule wa Vyombo vya Habari wa Mwaka 2015 yote kwa hati ya dharura.

Hata hivyo, miswada hiyo inalalamikiwa na wadau wa habari ambao wanapinga kuwasilishwa kwa hati ya dharura wakitaka iwasilishwe kwa mfumo wa kawaida ili wapate fursa ya kutoa maoni yao.

Awali, muswada wa takwimu uliwasilishwa kwenye mkutano wa 17 uliofanyika Novemba mwaka jana na baada ya wabunge kupinga vifungu vilivyoonekana kuwabana waandishi wa habari, serikali iliutoa bungeni kwa maelezo kuwa inaenda kuurekebisha.

Jana Bunge lilivyokaa kama kamati ili kupitisha muswada huo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alihoji juu ya kifungu hicho kinachotoa adhabu kali kwa waandishi wa habari wakati muswada huo huo unawalinda watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambao watatoa takwimu zisizo sahihi.

Baada ya mvutano mkubwa kati ya Mnyika na serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju (pichani), alisema muswada huo unawalinda watumishi wa NBS watakaotoa takwimu kwa makosa ‘kwa nia njema.’

Masaju alisema watakapopotosha taarifa hizo ukweli utajulikana mahakamani.

Mnyika alisema serikali haijafanya marekebisho yoyote kama ilivyokuwa imeahidi kwa kuwa adhabu bado ni kubwa bila sababu za msingi.

Waandishi wa habari wakiwa kazini barani Afrika

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya, alihoji iweje Serikali iweke kinga kwa mtumishi wa serikali anayetoa taarifa zisizo sahihi, lakini ikaacha kuweka kwa mwandishi anayepewa taarifa zisizo sahihi na ofisa huyo wa serikali na kuziripoti.

Akijibu hoja hiyo, Masaju alisema : “Ataenda kujieleza mahakamani ama polisi.”

Kabla ya kuondolewa bungeni Mwezi Novemba, Muswada huo pamoja na mambo mengine, ulikuwa ukipedekeza adhabu ya Sh. milioni 10 au adhabu isiyopungua kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa chombo cha habari kitakachotoa taarifa za kitakwimu za uongo au zenye upotoshaji.

“Mtu yeyote, kwa kujifanya anatimiza majukumu yake, iwapo anapata au anaomba kupatiwa taarifa ambayo haijaidhinishwa kuipata na kuichapisha au kuisambaza atakuwa amefanya kosa ambalo adhabu yake ni kifungo kisichopungua miezi 12 au fani isiyopungua Shilingi milioni mbili au vyote kwa pamoja,” kinasema kifungu cha 37 (d) cha muswada huo.

Muswada huo pia ulikuwa ukiainisha kwamba takwimu rasmi ni zile ambazo zimetolewa na kuidhinishwa na taasisi zilizoelezwa kwenye kifungu cha 20 cha muswada huo na ndizo pekee zinazoweza kutumika kama ushahidi kwenye kesi.

Adhabu kali pia zimependekezwa kwenye muswada huo kwa vyombo vya habari ambavyo vitatoa taarifa za takwimu zitakazosababisha watu wasishiriki kwenye shughuli zilizoandaliwa na serikali zinazohusiana na masuala ya takwimu.

Muswada huo unapendekeza pia adhabu kali kwa watu ambao watakataa kutoa ushirikiano kwa watu waliotumwa kufanya kazi za ukusanyaji taarifa kama vile sensa na adhabu iliyopendekezwa ni faini isiyopungua Shilingi milioni tano, kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.

Chanzo: NIPASHE

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE