
Mwapachu ni moja wa wasomi, na balozi mwenye heshima kubwa ndani na nje
ya nchi. Na kama kwa kweli ataondoka basi ni pigo kubwa sana kwa CCM, hasa
linapokuja suala la kumanage mabalozi wa nje. Mwapachu anaheshimika sana
na mabalozi wa nje hasa Marekani na nchi za Ulaya.
Hili hapa inasemekana ndiyo tamko la Mwapachu
Ndugu zangu,
Kesho ni siku muhimu katika kalenda ya Taifa letu. Tunamkumbuka marehemu
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyetutoka miaka 16
iliyopita. Nadhani ni siku mwafaka kwangu kufanya maamuzi magumu katika
maisha yangu ambayo yanahusu uanasiasa wangu. Mimi ni mwanachama wa CCM
tangu mwaka 1967 wakati nilipojiunga na TANU Youth League. Nimepata
fursa ya kuwa kiongozi ndani ya Chama hiki. Lakini kuanzia kesho mimi si
mwanachama wa CCM tena. Natoa maelezo yafuatayo:
Kwa kipindi chapata mwezi na nusu hivi sasa mmekuwa mkisoma makala zangu
kuhusu msimamo na mwelekeo wangu katika masuala ya siasa za hapa nchini
hususan kuhusu uchaguzi mkuu na mstakabali wa demokrasia nchini mwetu.
Nyote mnatambua kwamba kuanzia mchakato wa kumpata mgombe wa Urais ndani
ya CCM kule Dodoma, ambako nilipiga kambi, sijayumba katika msimamo
wangu kwamba Edward Ngoyai Lowassa ndiye chaguo langu katika kampeni za
kumpata Rais mpya wa Taifa letu.
Chaguo langu si ndoto wala mlipuko wa mapenzi juu ya Lowassa.
Nimemfahamu Lowassa tangu miaka ya 90 nikiwa cadre wa Chama cha
Mapinduzi kwa mahusisho katika majukumu ya Kichama. Lowassa amejaaliwa
nuru na uwezo wa kuongoza na wa kupendwa na watu. Ni msikivu pamoja na
kwamba ni kiongozi asiyependa ukiritimba na utovu wa nidhamu, iwe kwa
upande wa watumishi au wananchi wenyewe. Kubwa kwake ni ucha Mungu wake
ambao unamsaidia sana katika uongozi unaojali na kuheshimu utu, ukweli
na uwazi. Wanaodhani au kutaharuki kwamba eti anaweza au ana hulka ya
kulipiza kisasi kwa jambo lolote lile ni waongo; wanajilinda.
Lowassa ni chaguo la wengi na CCM, katika busara yake ya kumuengua
katika mchakato wa kumpata mgombea wa Urais, kimedhihirisha kutokuwa
Chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia. Dalili za Chama hiki
kupoteza lengo la kuwa Chama cha watu, na kuwa cha viongozi wachache
zilianza siku nyingi na hasa katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete. CCM kimebadilika na kuwa Chama cha makundi na
migawanyiko yakupambana, si kwa malengo ya itikadi na ujenzi wa Chama,
bali ya kumalizana na kutaka kufukuzana.
Lowassa angeweza kufukuzwa miaka mingi tu iliyopita! Aliweza kushinda
vita hivyo kutokana na kupendwa na wengi ndani ya CCM. Hivyo, kujitoa
kwake uanachama wa CCM hivi karibuni ni sahihi kabisa kwasababu CCM si
Chama tena cha watu. Kimetekwa. Na mimi nakubaliana na msimamo wa
Lowassa na hao waliyofuata kutoka nadani ya CCM.
Niliwahi kuandika makala katika ukurasa huu nikimnukuu mshairi mmoja wa
Uingereza aliyeandika kwamba, ‘there comes a time when the door opens
and allows the future in’. Mlango huo sasa umefunguka usoni mwangu na
huu uamuzi wangu maana yake ni kukubali kwamba wakati mpya umewadia; ni
wakati wa mabadiliko. Kuendelea kujihisi kwamba ningali mwana CCM wa
kadi ni kukubali kujidanganya mwenyewe. Si sawa. Kama marehemu Baba wa
Taifa alivyowahi kusema, ‘CCM si mama yangu’.
Hivyo ndugu zangu, kuanzia kesho mimi si mwana CCM tena. Nitarejesha
rasmi kadi yangu kupitia ofisi ya CCM ya kata yangu Mikocheni,
Dar-es-Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga na Chama kingine.
Mwenyezi Mungu anilinde.
Je! ni kweli hiyo kauli? Tutawaletea taarifa kamili juu ya tukio hilo pindi tukithibitisha.
Je! ni kweli hiyo kauli? Tutawaletea taarifa kamili juu ya tukio hilo pindi tukithibitisha.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment