
TAARIFA KWA UMMA
Hivi karibuni zimeibuka taarifa
zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zikimnukuu Waziri wa Nishati
na Madini, George B. Simbachawene akisema kuwa mitambo yote ya
uzalishaji umeme nchini inamilikiwa na Kampuni binafsi.
Tunapenda kuutaarifu Umma kuwa taarifa
hizi ni za uongo kwani Waziri Simbachawene hajawahi kutoa tamko la kuwa
mitambo ya kuzalisha Umeme yote nchini ni ya kampuni binafsi bali
alichosema ni kuwa, baadhi ya mitambo ni ya kampuni binafsi na mingine
inamilikiwa na Serikali.
Mitambo inayomilikiwa na Serikali ni:-
- Kinyerezi I (Gesi) yenye uwezo wa MW 150 ambapo MW 35 zimewashwa leo 12 Oktoba 2015;
- Ubungo I (Gesi) yenye uwezo wa MW 102 ambayo kwa sasa inazalisha MW 85;
- Ubungo II (Gesi) yenye uwezo wa MW 105 ambayo kwa sasa inazalisha MW 70;
- Tegeta (Gesi) yenye uwezo wa MW 42 ambayo kwa sasa inazalisha MW 42;
- Nyakato (Mafuta) yenye uwezo wa MW 60 ambayo kwa sasa inazalisha MW 42;
- Kidatu (Maji) yenye uwezo wa MW 204 ambayo kwa sasa inazalisha MW 27;
- Kihansi (Maji) yenye uwezo wa MW 180 ambayo kwa sasa inazalisha MW 45;
- Pangani (Maji) yenye uwezo wa MW 68 ambayo kwa sasa inazalisha MW 17;
- Nyumba ya Mungu (Maji) yenye uwezo wa MW 8 ambayo kwa sasa inazalisha MW 5;
- Hale (Maji) yenye uwezi wa MW 21 ambayo kwa sasa inazalisha MW 4; na
- Mtera (Maji) yenye uwezo wa MW 80 ambapo mitambo yake imezimwa (MW-0);
Kwa hiyo, Jumla ya kiasi cha umeme
kinachopatikana katika mitambo hiyo kwa sasa ni Megawati 337 kati ya
Megawati 870 zinazotakiwa kuzalishwa.
Mitambo inayomilikiwa na watu binafsi ni:-
- IPTL (Mafuta) yenye uwezo wa MW100 ambayo kwa sasa inazalisha MW 80;
- Aggreko (Mafuta) yenye uwezo wa MW 70 ambayo kwa sasa inazalisha MW 70;
- SONGAS(Gesi) yenye uwezo wa MW180 ambayo kwa sasa inazalisha MW 158; na
- Symbion (Gesi) yenye uwezo wa MW 112 ambayo kwa sasa inazalisha MW 74.
Hivyo mitambo hii ya watu binafsi inazalisha umeme wa kiasi cha Megawati 382 kati ya Megawati 462 zinazohitajika.
Ieleweke kuwa Serikali inajitahidi
kuiwasha mitambo hiyo yote inayomilikiwa na Serikali na Binafsi ili
izibe pengo la umeme wa maji ambao umepungua kutoka MW 561 hadi MW 88.
Ili nchi isiwe na mgawo wa umeme zinahitajika MW 1332 ambapo kwa sasa
kiasi cha umeme kinachopatikana ni Megawati 719.
Awali tulikuwa na upungufu wa megawati
takribani 450 lakini tumefanya juhudi za kuwasha mitambo mbali mbali
tangu wiki iliyopita na sasa upungufu uliobaki ni kati ya MW 200 na 250.
Serikali kupitia TANESCO inatoa rai kwa
Watanzania kuendelea kuvumilia kipindi hiki cha mpito kwani inajitahidi
kwa hali na mali kuwasha mitambo iliyobaki ya gesi ya Kinyerezi yenye
uwezo wa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 150 hivyo hadi ifikapo
tarehe 20 Oktoba, 2015 hali ya upatikanaji wa umeme itaanza kutengemaa.
Asanteni na poleni kwa usumbufu unaojitokeza.
Imetolewa na;
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
OCTOBER 13, 2015
0 MAONI YAKO:
Post a Comment