April 04, 2016

Bosi wa kamati ya usajili wa S imba, Zacharia Hans Poppe.
 
PAMOJA na kiwango kinachoonyeshwa na mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib, lakini bosi wa kamati ya usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Poppe amesema kuwa ‘dogo’ huyo hawezi kuichezea TP Mazembe ya DR Congo bali mfumo wao unamfaa  Simon Msuva wa Yanga.
Poppe amezungumza hayo katika ufafanuzi wa kuhusiana na ofa zinazosikika juu Ajib kutakiwa na mabingwa hao wa Afrika ambapo alieleza kutokana na falsafa ya Mazembe ni ngumu mchezaji huyo kuichezea timu hiyo.
Lakini akaenda mbali zaidi na kuingia kwenye kikosi cha mahasimu wao, Yanga na kumtaja Msuva kuwa ndiye mchezaji pekee kwa sasa anayeweza kuingia kwenye mfumo wa Mazembe na mwingine ni mshambuliaji wao, Danny Lyanga.
“Kuhusu ofa bado hatujapokea kutoka Mazembe lakini Ajib hatutegemei kutimkia Mazembe kutokana na aina ya soka analocheza, kupiga chenga nyingi, ku-control taratibu na kuweka ufundi mwingi.
“Unajua Mazembe aina ya mpira wao ni ule wa watu walioshiba, wajanja wa kupenya na wenye kasi ndiyo maana Ulimwengu (Thomas) bado anafanya vizuri na Samatta (Mbwana) alidumu kutokana na kufunga kwenye mazingira yoyote yale.
“Anayefaa kwa sasa kwenda huko ni Msuva wa Yanga na pengine Lyanga, wao wana hizo sifa za kuichezea Mazembe ambayo haina mpira wa kugusa-gusa. Lyanga ana nguvu na kasi na ni ngumu beki kuchukua mpira mguuni kwake. Msuva ana spidi na ni mjanjamjanja, hao wanaweza kufanikiwa,” alisema Poppe.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE