Kampuni hiyo iliingia mkataba na Jeshi la Polisi mwaka 2011 na kupewa zabuni ya Sh bilioni 37, kwa ajili ya kufunga mashine za alama za vidole katika vituo vya polisi, huku ikidaiwa kushindwa kutekeleza mkataba huo na hivyo kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema alisema Watanzania watajua ukweli kuhusu utapeli uliofanywa na kampuni hiyo dhidi ya Jeshi la Polisi.
Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), alisema kambi ya upinzani itahakikisha umma unapata ukweli juu ya sakata hilo, ambalo linaonekana kujumwisha baadhi ya vigogo wa Serikali.
Lema alisema nyaraka zinaonyesha kuwa mkataba huo ulisainiwa mwaka 2011 kati ya Kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi, ulikuwa ni kwa ajili ya kufunga mashine za utambuzi wa vidole katika vituo 108, kwa gharama ya Sh bilioni 37.
“Wakati mkataba wa kazi unasema hivyo, kampuni hiyo imefunga mashine katika vituo vya polisi 14 tu, huku kampuni hiyo ikilipwa Sh bilioni 34 za walipa kodi.
“Nikiwa msemaji wa wizara hii kupitia kambi ya upinzani, suala la Lugumi nitalishughulikia vizuri pale bungeni, hachomoki…vijana wa sasa wanasema nitakula naye sahani moja.
“Kampuni hii inaonekana wazi imesheheni watoto wa vigogo na makamishina wa Jeshi la Polisi, sitaki kukurupuka lakini ukweli wote ninao jambo hili halitazimika hata kidogo,” alisema Lema.
Alisema wakati wote wa mjadala juu ya sakata hilo amekuwa kimya na kusema kwamba ukimya wake unakishindo, kwani amelifuatilia kwa undani sakata hilo tangu lilipoanza.
“Suala hili ni zito limesemwa sana hadi kufikia hatua ya kupelekewa kwenye kamati za Bunge, lakini bado limeshindwa kujadiliwa,” alisema.
Alisema Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ina mamlaka kamili ya kufanya mambo yote, bila kushurutishwa, lakini anashangaa kuona katika suala hilo kamati hiyo imekosa makali.
“Kamati hii imepewa mamlaka kamili ya kusimamia na kushughulikia masuala yote yanayohusu fedha za Serikali na hapa kuna ufisadi wa mabilioni ya fedha, …inawezekana vipi iitishe mkataba halafu iporwe na kamati nyingine?
“Sitaki kueleweka vibaya, makamu mwenyekiti wa ile kamati hana uwezo, siku zote kamati inapaswa kuongozwa na mpinzani…kwa mtindo huu unategemea nini?
“Inatakiwa mwenyekiti ambaye anaweza kuchambua na kuelewa mambo kwa mapana zaidi, anatakiwa mtu nyeti badala yake walipanga kamati wanavyotaka wenyewe.
“Hapa ndiyo maana nahoji uadilifu wa Rais John Magufuli uko wapi katika suala zito kama hili…amejipambanua ni kiongozi wa kupambana na ufisadi, rushwa nilitegemea angekuwa wa kwanza kuhoji au kutoa tamko juu ya sakata hili.
“Unajua hata Mungu ameumba ndege wengi, wapo wenye mabawa marefu, mafupi, wanaokula sana na wengine kidogo…maana yake ni kwamba kuna maeneo lazima yashikwe na wapinzani,” alisema Lema.
Alisema kutokana na mwenendo wa suala hilo, ni wazi kamati za Bunge zimeanza kutoa nafasi kubwa ya kuchezewa tofauti na miaka ya nyuma.
“Huu ni mwanzo wa kuchezea kamati za Bunge, siku zote mambo haya hupikwa huko kabla ya kupelekwa pale bungeni…nasema tumejipanga katika hili,”alisema Lema.
Huku akionekana kukerwa na usiri wa mkataba huo, Lema alisema suala hilo ni kubwa mno kwa sababu inaonekana linagusa maslahi ya wengi.
“Namwomba sana Rais Magufuli asiendelee kukaa kimya, najua ana ujasiri mkubwa au kuna baadhi ya mambo anayoogopa? nadhani anapaswa kutoa mwelekeo.
“Kampuni ya Lugumi ina vigogo, yeye ni nani, tutabana maisha yake ya mbwembwe na sifa nyingi mjini hachomoki tutakula naye sahani moja,” alisema Lema.
Sakata lilivyoanza
Aprili 6, mwaka huu Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Aeshi Hilaly walibaini utata mkubwa wa utekelezaji wa mkataba huo na kuagizwa upelekwe mbele ya kamati hiyo ili wajumbe waweze kujadili.
PAC iligundua madudu hayo, wakati watendaji wa Jeshi la Polisi walipokuwa wakihojiwa na kamati hiyo juu ya utendaji wa shughuli zao.
Baada ya hapo, kumekuwa na taarifa nyingi zakiwamo za kutoka Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Bunge ya Bunge kuwa kilichombwa na PAC ni taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo na si mkataba wenyewe.
CUF
Kwa upande wake Chama cha Wananchi (CUF), kimewataka wabunge kuhakikisha wanaipitia kwa umakini Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na endapo hakutakuwa na maelezo ya kina kuhusu kashfa ya ufisadi wa Kampuni ya Lugumi waipinge.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho (Bara), Abdul Kambaya alisema haiwezekani mabilioni ya Watanzania yakapotea bila maelezo ya kina.
Alisema Serikali inapaswa kueleza matumizi ya Sh bilioni 37 ambazo zilitakiwa zitumike kwa ajili ya kufunga mashine za utambuzi wa alama za vidole katika vituo vya polisi zaidi ya 100 nchini kote, lakini hadi sasa ni vituo 14 tu vilivyofungwa na havijulikani vilipo vituo hivyo.
Kambaya alisema katika sakata hilo kuna harufu ya ufisadi lakini hadi sasa hakuna maelezo ya kina yanayotolewa kuhusu Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni hiyo.
“Wabunge mnahaki ya kupinga bajeti hiyo kama hamtapata maelezo ya kina kuhusu kampuni hiyo na matumizi ya fedha hizo, naomba mchukue hatua kwa kuwa fedha hizo ni zetu na zingeweza kusaidia sekta nyingine,”alisema Kambaya.
Aliongeza kuwa, wabunge waangalie kwa makini na kuzipa kipaumbele bajeti ambazo zimetoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu, afya na miundombinu.
Kambaya alisema Watanzania wanahitaji kubadili mfumo wa uongozi hapa nchini ili kila mmoja aweze kutoa mawazo yake na uamuzi uwe wa ushirikishwaji baina ya watu wote.
Pia alisema alimwomba Rais Dk.John Magufuli kuingilia kati na kuchukua uamuzi stahiki kuhusu sakata la umeya wa Jiji la Tanga ambalo bado linatia shaka.
“Ni vema wabunge suala la umeya wa Jiji la Tanga mlizungumze kwa umakini pindi mtakapoanza vikao vya Bunge ili tupate majibu ya kueleweka kama ilivyotokea hapa Dar es Salaam,”alisema Kambaya.
Kwa upande wake, mchambuzi wa mambo ya siasa Julius Mtatiro alisema anaishangaa serikali kutenga bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ya Sh bilioni 100 kwa mwaka 2016/2017 wakati ujenzi wa kiwanda cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara kimetumia Sh bilioni 1000, hivyo itatumia muda wa miaka 10 kwa Tanzania kujenga kiwanda kimoja.
Alisema nchi haina viwanda na hakuna jitihada zinazofanyika hivyo majipu yataendelea kutumbuliwa lakini matatizo yatazidi kuongezeka.
“Bila kuongeza jitihada kwenye sekta ya viwanda vijana wengi wataishia mitaani kwakuwa Serikali ina uwezo wa kuajiri kila mwaka watu 50 kitakachofanyika maeneo mengi yatakuwa hayana huduma muhimu,”alisema Mtatiro.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) alisema Serikali lazima ijipange kuwasaidia waathirika wa mabondeni kwa kuwalipa fidia.
Alisema wananchi wa Kinondoni wa Mto Ng’ombe waliowekewa alama ya X nyumba zao haziwezi kubomolewa hadi watakapolipwa fidia.
“Tumejipanga kama nyumba zitabomolewa ni lazima wananchi walipwe fidia zao na kwa wale waliovunjiwa bila fidia tutafungua kesi mahakamani,”alisema Mtulia.
Naye Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF) alisema Magufuli anatumbua vipele wao wataenda kutumbua majipu bungeni.
Wakati huohuo, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Bonifas Jacob alisema kuanzia sasa wananchi wa Kinondoni watanufaika na huduma za bure kwa kupata huduma za afya bure.
Alisema wananchi hao watalipa Sh 40,000 kwa mwaka ambapo wataenda katika hospitali za serikali pamoja na zahanati kupata huduma za afya.
Jacob alisema wazee 34,000 watanufaika na huduma za afya bure ambapo watatambuliwa kila mtaa na kupewa kadi maalum za matibabu.
Kwa upande wa wajumbe wa mtaa sasa watalipwa Sh 30,000 kila mwezi badala ya Sh 5,000 na wenyeviti wa serikali za mitaa watapewa Sh 100,000 kwa mwezi badala ya Sh 50,000 waliyokuwa wakilipwa awali.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment