
KATIBU mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amemaliza ziara yake nchini Marekani na kuelekea Canada.
Maalim Seif alihitimisha ziara yake hiyo kwa mkutano wa hadhara
ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na Watanzania waishio nchini humo.
Katika mkutano huo, mwanasiasa huyo alisema kuwa lengo la ziara yake
ni kuuelezea ulimwengu kuhusu kile kilichotokea Zanzibar kutokana na
uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 na mwelekeo wa demokrasia nchini Tanzania
kwa ujumla.
Alisema ziara yake nchini Marekani imezaa matunda. “Sina budi
kumshukuru Mwenyezimungu kuwa tumeeleweka na ziara yetu imezaa matunda,”
alisema Maalim Seif ambaye alikua mgombea urais wa Zanzibar katika
uchaguzi huo.
Akizungumzia zoezi la uchaguzi wa mwaka jana visiwani Zanzibar,
Maalim Seif alisema uchaguzi huo ulihudhuriwa na waangalizi wa kimataifa
na wa ndani.
“Waangalizi wote, wote kabisa, walikiri kuwa uchaguzi ulikuwa huru na
wa haki. Ulikuwa uchaguzi bora kabisa kuliko chaguzi zote
zilizotangulia Zanzibar,” alisistiza Maalim Seif
Alisema mchakato wa uchaguzi kuwa ulikwenda vizuri mpaka kufikia
Oktoba 27, jumla ya majimbo 34 ya uchaguzi yalikuwa tayari
yameshatangazwa na mengine tisa yakiwa yameshahakikiwa ikiwa bado
kutangwazwa .
“Na kwa upande wa udiwani na uwakilishi, uchaguzi ulikuwa umeshakamilika na washindi kupewa shahada zao za ushindi.
“Kufika hapo tukashuhudiwa vituko vya Tume ya Uchaguzi hususan mwenyekiti wake”, alisema Maalim Seif,
Maalim Seif, alisema kitendo cha Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, cha kufuta uchaguzi huo kinakiuka sheria za uchaguzi.
Pamoja na hali hiyo, alisema alichukua hatua kadhaa ikiwemo za
kujaribu kutatua mgogoro huo, ambapo moja ya hatua hizo muhimu ni
kuwasiliana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia
alikuwa mgombea wa urais.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment