Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
29 Juni, 2016 amewaapisha wakuu wa Mikoa watatu aliowateua Jumapili
iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.
Wakuu
wa Mikoa walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es salaam ni Dkt. Binilith
Satano Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Charles Ogesa
Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara na Bi. Zainab Rajab Telack ambaye
ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Hafla
ya kuapishwa kwa wakuu hao wa Mikoa imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, wakuu
wa vyombo vya ulinzi na usalama na wakuu wa wilaya wateule ambao
waliteuliwa na Rais Magufuli Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.
Aidha,
miongoni mwa wakuu wa wilaya 139 walioteuliwa, Rais Dkt. John Pombe
Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika wilaya tatu ambapo ametengua
uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mteule Mhe. Fatma Hassan Toufiq na
badala yake amemteua Bi. Agness Elias Hokororo kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo,
ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mteule Bw. Emile Yotham
Ntakamulenga na badala yake amemteua Bw. Nurdin Hassan Babu kuwa Mkuu
wa Wilaya hiyo na ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mteule
Bw. Fikiri Avias Said na badala yake amemteua Bw. Miraji Mtaturu kuwa
Mkuu wa wilaya hiyo.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amewataka wakuu wa wilaya wateule kwenda kuchapa kazi na
kutatua kero za wananchi katika wilaya zao huku wakizingatia kufanya
kazi kwa uadilifu na uaminifu.
Rais
Magufuli pia amewataka kusimamia ukusanyaji mapato ya serikali na
matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma, kuhakikisha wananchi
wapo salama na pia kuhakikisha wananchi wanafanya kazi za uzalishaji
mali.
“Katika
kazi hizi wapo watakaowakejeli, katika kazi hizi wapo watakaowadhihaki,
nyinyi kavumilieni na mmuweke Mungu mbele na mkawaweke watanzania
mbele, mkafanye kazi kadiri Mungu atakavyokuwa amewaongoza.
“Nataka
kuwahakikishia tunawaunga mkono kwa nguvu zote, mkafanye kazi bila
uwoga wowote, katembeeni kifua mbele, kwa sababu tumewaamini wala msiwe
na wasiwasi, ukifanya kitu kizuri kwa dhamira yako iliyo njema kitazaa
matunda mazuri, ukifanya kitu kwa unafiki hakitafanikiwa” Amesema Rais Magufuli
Katika
hafla hiyo, wakuu wa mikoa walioapishwa na wakuu wa wilaya wateule
wamekula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo
limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda.
Katika hatua nyingine,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amekutana na kufanya Mazungumzo na mwenyekiti mwenza wa taasisi ya Bill
and Melinda Gates ya Marekani Bi. Melinda Gates ambapo Rais Magufuli
amemuhakikishia mwenyekiti mwenza huyo kuwa serikali ya awamu ya tano
itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na taasisi hiyo ambayo
imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya Afya, Uongozi na Kilimo.
Kwa
upande wake Bi. Melinda Gate amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa
anayoifanya katika kukabiliana na rushwa na kuongeza ukusanyaji wa
mapato ya serikali, na pia kwa nia yake thabiti ya kuinua sekta ya
kilimo inayotegemewa na idadi kubwa ya watanzania na ameahidi kuwa
taasisi ya Bill and Melinda Gates itaendelea kushirikiana na Serikali ya
awamu ya tano katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
29 Juni, 2016
0 MAONI YAKO:
Post a Comment